brightness_1
KURUDIA DUA NA KUOMBA KWA MSISITIZO.
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Ibniabass –RAA-ambayo imetangulia kutajwa ambapo Mtume -SAW- amenukuliwa kusema kuwa: “Ewe Mola wangu, nitimizie uliyoniahidi. Ewe Mola wangu, nipe uliyoniahidi”. Mtume hakuacha kumuomba Mola wake mpaka Kashida yake ikamuanguka, na Abubakar akiwa nyuma yake akimwambia: “Ewe Mtume wa Allah, yanatosha ulivyomuomba Mola wako”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (1763).
Na vilevile kuna Hadithi katika Swahiih Bukhaari na Swahiih Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira -RAA- kwamba, Mtume -SAW- alipowaombea (kabila la) Daus, alisema: “Ewe Mola wangu, waongoze Daus na walete. Ewe Mola wangu, waongoze Daus na walete”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (2937), na Muslim kwa nambari (2524).
Na vilevile kuna Hadithi katika Swahiih Muslim kuhusu: “Mtu anayesafiri safari ndefu, akiwa kachafuka, kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akiomba: “Ewe Mola wangu! Ewe Mola wangu”. Ameipokea Imamu Muslim kwa nambari (1015). Huku ni kurudia ambako ndani yake kuna msisitizo.
Na Suna ni kuomba mara tatu, kwa mujibu wa Hadithi ya Ibnimasoud -RAA- iliopo katika Swahiih Bukhaari na Swahiih Muslim). Ndani ya Hadithi hiyo kuna nukuu kwamba, “Anapo omba alikuwa anaomba mara tatu, kisha anasema: “Ewe Mola wangu, wakamate (wadhibiti) Wakuraishi” mara tatu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (240) na Muslim kwa nambari (1794).