Ufafanuzi wa mambo ambayo ni Suna Muislamu kuyafanya anapotaka kuomba Dua. Ni katika Suna:
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abumusa -RAA- iliopo katika Swahiih Bukhaariy na Swahiih Muslim, na kisa chake yeye na ami yake Abuamir -RAA- pale Mtume -SAW- alipomtuma kwenda kupambana na jeshi la Autwaas. Katika Hadithi hiyo kuna nukuu kwamba: “Abuamir-RAA- aliuawa na (kabla ya kuuawa) alimuusia Abumusa –RAA- amsalamie Mtume -SAW- na kumuomba amuombee Dua. Abumusa -RAA- akasema: Nikamhabarisha Mtume habari yetu na habari ya Abuamir, na kumwambia: Amesema Abuamir: Mwambie Mtume aniombee maghfirah. Mtume –SAW- akaagiza aletewe maji. Alitawadha, kisha akainua mikono yake, kisha akasema: “Ewe Mola wangu, mghufirie Abeid Abuamir” mpka nikaona weupe wa kwapa zake. Kisha Mtume akasema: “Ewe Mola wangu, mjaalie Siku ya Kiama awe juu ya viumbe wako wengi, au juu ya watu wengi”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (4323) na Muslim kwa nambari (2498).
Imenukuliwa kwa Abdallah bin Abbas –RAA- akisema kuwa: “Amenisimulia Umar bin Khatwab -RAA- na kusema: Ilipokuwa siku ya (vita vya) Badri, Mtume –SAW-aliwaangalia Makafiri wakiwa elfu moja, na Swahaba zake wakiwa watu mia tatu na kumi na tisa. Mtume wa Allah akaelekea Kibla, kisha akanyanyua mikono yake akaanza kumuomba Mola wake: Ewe Mola wangu, nitimizie uliyoniahidi. Ewe Mola wangu, nipe kile ulichoniahidi. Ewe Mola wangu, kikiangamia hiki kikundi cha Waislamu wachache hutoabudiwa katika ardhi. Mtume aliendelea kumuomba Mola wake huku akiwa amenyanyua mikono yake na kuelekea Kibla, hadi Kashida yake iliyokuwa mabegani ikamdondoka. Abubakar akamfuata Mtume, akaokota Kashida kisha akaitupia katika mabega ya Mtume. Kisha Abubakar akasimama nyuma ya Mtume na kumwambia: “Ewe Mtume wa Allah, yatosha ulivyomuomba Mola wako. Hakika, atakutimizia alichokuahidi”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (1763).
Kwa mujibu wa Hadithi aliyoipokea Tirmidhi akimnukuu Fudhala bin Abeid- RAA- aliyesema kuwa, wakati Mtume –SAW- akiwa ameketi, aliingia mtu mmoja na kuswali kisha akasema: “Ewe Mola wangu, nisamehe na nirehemu” Mtume-SAW- akasema: “Umefanya haraka ewe mwenye kuswali. Unaposwali na kuketi, mhimidi Allah kwa sifa zake anazostahiki, kisha niswalie, kisha muombe Allah”. Imepokewa na Tirmidhi kwa nambari (3476), na Shekhe Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Swahiihuljaamiu 1/172).
Mtu achague katika majina ya Allah yale majina yaliyo mazuri kulingana na maudhui ya dua yake. Akimuomba Allah riziki aseme: “Yaa Razzaaq” (Ewe Mwenye kuruzuku). Akimuomba Allah –SWT- rehema aseme: “Yaa Rahmaan, Yaa Rahiim” (Ewe Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu). Akimuomba Allah nguvu na utukufu aseme: “Ya Aziiz” (Ewe Mwenye ezi). Akimuomba Allah maghfira aseme: “Yaa Ghafuur” (Ewe Mwingi wa kusamehe). Akimuomba Allah kupona ugonjwa aseme: “Yaa Shaafii” (Ewe Mwenye kuponya).
Aombe kwa kutumia majina (ya Allah) yanayonasibiana na maombi yake, kwa mujibu wa kauli ya Allah isemayo kuwa: {Na Allah ana majina mazuri kabisa, hivyo muombeni kwayo}. (Sura Al-aaraaf: 180).
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Ibniabass –RAA-ambayo imetangulia kutajwa ambapo Mtume -SAW- amenukuliwa kusema kuwa: “Ewe Mola wangu, nitimizie uliyoniahidi. Ewe Mola wangu, nipe uliyoniahidi”. Mtume hakuacha kumuomba Mola wake mpaka Kashida yake ikamuanguka, na Abubakar akiwa nyuma yake akimwambia: “Ewe Mtume wa Allah, yanatosha ulivyomuomba Mola wako”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (1763).
Na vilevile kuna Hadithi katika Swahiih Bukhaari na Swahiih Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira -RAA- kwamba, Mtume -SAW- alipowaombea (kabila la) Daus, alisema: “Ewe Mola wangu, waongoze Daus na walete. Ewe Mola wangu, waongoze Daus na walete”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (2937), na Muslim kwa nambari (2524).
Na vilevile kuna Hadithi katika Swahiih Muslim kuhusu: “Mtu anayesafiri safari ndefu, akiwa kachafuka, kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akiomba: “Ewe Mola wangu! Ewe Mola wangu”. Ameipokea Imamu Muslim kwa nambari (1015). Huku ni kurudia ambako ndani yake kuna msisitizo.
Na Suna ni kuomba mara tatu, kwa mujibu wa Hadithi ya Ibnimasoud -RAA- iliopo katika Swahiih Bukhaari na Swahiih Muslim). Ndani ya Hadithi hiyo kuna nukuu kwamba, “Anapo omba alikuwa anaomba mara tatu, kisha anasema: “Ewe Mola wangu, wakamate (wadhibiti) Wakuraishi” mara tatu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (240) na Muslim kwa nambari (1794).
Kwa mujibu wa kauli ya Allah –SWT- isemayo kuwa: {Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri….}. (Sura Al-aaraf: 55). Kuomba dua kwa siri kuna uhalisia zaidi wa kumkusudia Allah (Ikhlasi). Kwa sababu hiyo, Allah amemsifu Zakaria -AS- na kusema: {Alipomuomba Mola wake maombi ya siri} [Sura Maryam: 3] akitafuta ikhlasi kwa mujibu wa moja ya kauli za wanazuoni wa Tafsiri ya Kurani.
Faida: Baadhi ya watu wanaweza kuuliza: Niseme nini katika Dua yangu?
Jawabu ni kwamba: Omba unachotaka, katika mambo ya dunia na ya akhera. Na katika dua yako jitahidi kutumia maneno yanayojumuisha maana nyingi. Hizi ni dua ambazo zimo katika Kurani na Suna. Ndani ya Dua hizo kuna kuomba mema ya duniani na akhera. Hebu tafakari hili swali aliloulizwa Mtume –SAW- naye akalijibu kwa kutumia maneno makubwa, yenye kumkusanyia Mwislamu dunia na akhera. Ni bishara kubwa sana, na ni tunu iliyosheheni. Tumia Dua hizo na zitie akilini.
Imenukuliwa kwa Abumalik Al-ashjai naye akimnukuu baba yake –RAA- kwamba “Alimsikia Mtume –SAW- akiwa amefuatwa na mtu aliyeuliza hivi: Ewe Mtume wa Allah, Vipi niseme pindi ninapomuomba Mola wangu? Mtume akasema: “Sema: Ewe Allah, nighufurie na nirehemu na nipe uzima na niruzuku, na (Mtume alikuwa) anakusanya vidole vyake pomoja ila dole gumba. (Mtume aliendelea kusema): Hakika, maneno haya yanakukusanyia dunia yako na akhera yako”. Imepokelewa na Muslim kwa nambari (2697).
Na katika mapokezi mengine ya Imam Muslim kuna nukuu kwamba: “Mtu alipokuwa anaingia katika dini ya Kiislamu, Mtume –SAW- alikuwa anamfundisha Swala, kisha anamuamrisha kuomba dua kwa kutumia maneno haya: “Ewe Allah, nighufurie na nirehemu na niongoze na nipe uzima na niruzuku”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2697).
Faida nyingine: Ni Suna kwa mwanadamu kumuombea dua ndugu yake ambaye hayupo naye. Hii ni dua yenye kujibiwa, kwa uwezo wa Allah-SWT-. Mwenye kuombea naye anapata fadhila kubwa ambazo zimeelezwa katika Hadithi aliyoipokea Imamu Muslim katika kitabu chake cha Swahiih Muslim akimnukuu Abudardai - RAA- kwamba, Mtume -SAW- amesema kuwa: “Maombi ya Muislamu kwa nduguye akiwa hayupo naye ni yenye kujibiwa. Kwenye kichwa chake kuna Malaika aliyepewa kazi maalumu. Kila Muislamu atakapomuombea kheri ndugu yake, Malaika yule anasema: Aamin, nawe upate kama hayo (uliyomuombea nduguyo)”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2733).