Ni Suna kwa mwenye kuingia chooni, aseme zile nyiradi zilizonukuliwa kwa Mtume na ambazo zipo katika Swahiih Bukhaarii na Swahiih Muslim:
Imenukuliwa kwa Anas –RAA- kwamba, “Mtume wa Allah -SAW- anapoingia chooni alikuwa anasema: “Allaahuma Innii Auudhubika Minalkhubuthi Walkhabaa-ith au Minalkhub-thi” (Ewe Allah, Hakika mimi ninakuomba kinga dhidi ya majini wa kiume na majini wa kike au unikinge dhidi ya uovu). Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6322) na Muslim kwa nambari (375).
Maombi ya kinga ni dhidi ya mashetani wa kiume na wa kike.
Na (Uovu) ni nafsi zenye shari. Kwa hiyo, maombi ya kinga ni dhidi ya shari na wenye shari. Na nukuu hii ina maana pana zaidi.
Ni Suna kwa anayetoka chooni aseme:
Uradi uliopokewa katika Hadithi iliopo katika kitabu cha Musnad Ahmad, Sunan Abiidaauud na Tirmidhiy, na Shekh Albani amesema kuwa ni sahihi. Imenukuliwa kwa Aisha–RAA- kwamba, amesema kuwa: “Mtume –SAW- anapotoka chooni alikuwa anasema “Ghufraanaka” (Naomba msamaha wako (Ewe Allah)” Imepokewa na Ahmad kwa nambari (25220), Abudaud kwa nambari (30) na Tirmidhi kwa nambari (7). Shekhe Albani na amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Tahqiiqu Mishkaatilmaswaabiih 1/116).
Kuandika wasia ni Suna kwa kila Muislamu akiwa mgonjwa au mzima, kwa mujibu wa kauli ya Mtume -SAW-kwamb: “Si haki kwa mtu Muislamu ambaye ana jambo analotaka kulitolea usia, alale siku mbili bila ya wasia wake kuwa anao (na) umeandikwa”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (2783) na Muslim kwa nambari (1626) ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Ibniumar-RAA-. Na kutajwa siku mbili katika Hadithi sio kwamba imefungika. Kinachokusudiwa ni kuwa, usimpitikie mtu muda mfupi isipokuwa wasia wake awe nao umeandikwa, kwa sababu hajui atakufa lini. Suna hii ni ya watu wote.
Ama wasia katika mambo ambayo ni haki ya Allah -SWT- kama Zaka, Hija, au Kafara au haki za binadamu, kama deni, kutekeleza amana za watu, ni wajibu na sio Suna, kwa sababu unafungamana na utekelezaji wa haki ambazo ni wajibu, hasa kama hakuna yeyote anayejua haki hizi ] Na jambo ambalo wajibu hautimii ila kwalo, nalo ni wajibu [.
Hilo linapatikana kwa kila mmoja kati ya muuzaji na mnunuzi kuwa na sifa ya kusamehe na upole wakati wa kuuza au kununua. Mmoja wao amsifanyie ugumu mwenzake katika kupatana bei na kuwa mbishi katika hilo. Lakini wanatakiwa wanasameheane.
Na hoja ya hili ni:
Hadithi ya Jabir bin Abdallah-RAA- kwamba, Mtume wa Allah –SAW-amesema kuwa: “Allah amrehemu mtu msamehevu anapouza, na anaponunua, na anapodai”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (2076).
Pia mtu anapodai kulipwa haki yake, ni katika Suna adai kwa wepesi na upole, kwa mujibu wa kauli ya Mtume –SAW-:“Na anapodai”.
Hii ni katika Suna za kila siku ambazo zina ambatana na fadhila kubwa, ambayo ni kuingia Peponi. Imepokewa kwa Abuhuraira –RAA- kwamba: “Mtume–SAW-alimwambia Bilali wakati wa swali ya Alfajiri kwamba: “Ewe Bilali, niambie amali unayotarajia sana malipo yake ambayo umeifanya katika Uislamu, kwa sababu mimi nimesikia mlio wa viatu vyako mbele yangu peponi”. Bilali akasema: “Sikufanya amali ambayo nina matarajio nayo isipokuwa kwamba sikujitwaharisha tohara yoyote usiku au mchana ila niliswali kwa tohara hiyo nilichojaliwa kuswali”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (1149) na Muslim kwa nambari (2458).
Kusubiri swala ni katika Suna ambazo zina fadhila kubwa.
Na hoja ya hilo ni:
Hadithi ya Abuhuraira -RAA- kwamba, Mtume (SAW) amesema kuwa: “Mmoja wenu ataendelea kuwa katika swala madamu swala inamfunga (kwa maana kwamba) hakuna kilichomzuia kwenda kwa familia yake isipokuwa swala tu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (659), na Muslim kwa nambari (649). Mtu kwa kungoja kwake (kuswali) anapata ujira wa swala.
Na imepokewa kwa Abuhuraira –RAA- kwamba, Mtume wa Allah amesema kuwa: “Malaika wanamuombea rehema mmoja wenu madamu yungali katika sehemu yake ya kuswalia, na madamu hajauvunja udhu wake. (Malaika wanaomba) Ewe Allah, msamehe. Ewe Allah, mrehemu. Mmoja wenu ataendelea kuwa katika swala madamu swala imemfunga, (kwa maana kwamba) hakuna kilichomuzuii kwenda kwa familia yake ila swala tu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (659), na Muslim kwa nambari (649). Na kauli ya Mtume kwamba: “Madamu hajavunja udhu wake” ina maana madamu hajafanya jambo lenye kutengua udhu. Na imekuja nukuu kwa mapokezi ya Muslim kwamba:
“Madamu hajaudhi ndani yake, madamu haja pata la kutengua Udhu ndani yake”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (649). Maana ni kwamba, thawabu hizi katika kuzipata zimewekewa sharti kuwa, asimuudhi mtu yeyote hapo alipokaa na Udhu wake usitenguke.
Kupiga mswaki ni katika Suna ambazo hazifungamani na wakati; na ambazo hufanywa wakati wowote. Mtume –SAW - alikuwa akisisitiza sana kupiga mswaki mpaka akasema: “Nimekithirisha sana kukuambieni kuhusu mswaki”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (8888) ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Anas –RAA-. Pia Mtume –SAW- amesema kuwa: “Mswaki ni kisafisha mdomo na ni kiridhisha Mola”. Ameipokea Ahmad kwa nambari (7) na Nasai kwa nambari (5) ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Aisha- RAA-, na Shekhe Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Al-irwaa 1/105).
Na Suna ya kupiga mswaki inasisitizwa zaidi katika sehemu ambazo baadhi yake zimetangulia kutajwa, hasa zile ambazo zinajirudiarudia katika siku, kama kisimamo cha usiku, wakati wa kutawadha, wakati wa kila swala na wakati wa kuingia nyumbani. Allah ndiye Mjuzi zaidi.
Ni Suna kwa Muislamu kurudia upya kutawadha kwa kila swala. Kama mtu alitawadha kwa ajili ya swala ya Magharibi, kwa mfano, kisha akaswali Magharibi. Ikija swala ya Isha, ni Suna kwake kutawadha hata kama Udhu anao. Suna ni mtu kutawadha udhu mpya kwa kila swala.
Na hoja ya hilo ni:
Hadithi iliopo kwa Bukhari aliyenukuu na kusema kwamba: “Mtume-SAW- alikuwa anatawadha wakati wa kila swala”. Imepokewa na Bukhari (214).
Pia ni katika Suna mtu kuwa na twahara siku yake yote, kwa mujibu wa Hadithi ya Thauban -RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume –SAW- amesema kwamba: “Na hadumu kuwa na Udhu ila mtu mumini tu”. Imepokewa na Ahmad kwa nambari (22434), Ibnimaja kwa nambari (277), Daarimi kwa nambari (655), na Shekhe Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Swahiihuljaamiu 1/225).