Na hoja ya Suna hii ni nyingi mno. Miongoni mwa hoja hizo ni: Hadithi ya Abuhuraira -RAA- akinukuliwa kusema kwamba, Mtume-SAW- amesema kuwa: “Haki za Muislamu kwa Muislamu (mwenzake) ni sita. Mtume aliulizwa: Ni zipi haki hizo ewe Mtume wa Allah? Mtume akasema: Ukikutana naye msalamie, na akikualika muitikie, na akikutaka ushauri mshauri, na akipiga chafya akamhimidi Allah (yaani akasema Alhamdulillaah), muombee Rehema (Mwambie: Yarhamukallaahu), na akiugua mtembelee, na akifa sindikiza jeneza lake”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2162).
-Ama kujibu Salamu ni: wajibu. Na hoja juu ya hili ni:
Kauli ya Allah Mtukufu isemayo kuwa: {Na mtakapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, itikieni kwa maamkizi yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika, Allah daima ni Mwenye kuhesabu kila kitu}. (Sura Annisaa: 86).
Na asili katika amri ni lazima, madamu amri hiyo haijaondolewa na cha kuiondoa (katika ulazima). Wanazuoni wengi wamenukulu makubaliano juu ya wajibu wa kujibu Salamu. Miongoni mwa wanazuoni hao ni Ibnihazmi, Ibniabdulbari, Sheikh Taqiyyudiin na wengine – Allah awarehemu wote-. Angalia: Al-aadaab Ash-shar-iyya (1/356), chapisho la Mu-assasaturrisaala.
-Na tamko bora na kamilifu mno la kusalimu na kujibu Salamu ni: (Assalaamu Alaykum Warahmatullaahi Wabarakaatuh = Amani iwe kwenu na rehema za Allah na Baraka zake). Tamko hii ndio salamu bora zaidi na timilifu zaidi.
Ibnulqayyim –Allah amrehemu- amesema kuwa: “Na muongozo wa Mtume -SAW- ulikuwa kuishia Salamu mpaka: (Wabarakatuh)”. Angalia: Zaadul Ma’ad (417/2).
Na kutangaza Salamu sio kwamba ni Suna tu, lakini pia ni Suna iliyotiwa ushawishi kwamba ina fadhila kubwa, kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhurara -RAA- akinukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah-SAW- amesema kwamba: “Nina apa kwa (Allah) ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hamtaingia Peponi hadi muamini. Na hamuwezi kuamini hadi mpendane. Je, nikufahamisheni jambo ambalo mtakapolifanya mtapendana? Tangazeni Salamu baina yenu”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (54).
Kama vile mtu kuwa na shaka kwamba, aliyemsalamia hakusikia alipomsalamia mara ya kwanza. Hapo, inapendekezwa arudie mara ya pili. Na kama hakusikia, arudie mara ya tatu. Ni kama hivyo mtu akiingia pahala penye mjumuiko wa watu wengi; kama vile mtu kuingia katika kikao kikubwa chenye watu wengi. Akisalimia mara tu pale mwanzo anapoingia, hawatasikia salamu hiyo isipokuwa tu wale walioko mwanzoni. Katika hali hiyo. inahitajika asalamie mara tatu ili wasikie watu wote walio katika kikao.
Na hoja juu ya hili ni Hadithi ya Anas –RAA- akinukuu kwamba, Mtume –SAW-: “Mtume alikuwa akiongea neno hulirudia mara tatu; mpaka lifahamike. Na akiwajia watu na kuwasalamia, huwasalamia mara tatu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (95).
Na inachukuliwa katika Hadithi ya Anas -RAA- iliyotangulia kwamba ni Suna kurudia neno mara tatu kama kutakuwa na haja ya kufanya hivyo, kama mtu kuzungumza na maneno yake yakawa hayajafahamike. Ni Suna kurudia, na kama hayajafahamika arudie mara tatu.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abdallah bin Amri –RAA- kwamba: “Mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allah kwamba: Uisilamu upi ni bora? Mtume akasema: “lisha chakula, na msalimie unayemjua na usiyemjua”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (12), na Muslim kwa nambari (39).
Imenukuliwa kwa Abuhuraira –RAA- akisema kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema: “Aliyepanda (chombo cha usafiri) amsalimie anayetembea kwa mguu, na mwenye kutembea kwa mguu amsalimie aliyeketi, na wachache wawasalamie wengi”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari: (6233) na Muslim kwa nambari (2160). Na katika mapokezi ya Bukhari kuna nukuu kwamba: “Mdogo amsalimie mkubwa, na mwenye kupita amsalimie aliyekaa, na wachache wawasalamie wengi”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (6234).
Kufanya tofauti ya utaratibu bora katika kusalimia haimaanishi kwamba ni makruhu. Hakuna ubaya kufanya hivyo, lakini ni kufanya tofauti iliyo bora; kama mkubwa kumsalamia mdogo, mwenye kutembea kwa miguu kumsalimia aliye katika chombo cha usafiri, na mfano wa hivyo.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Anas bin Malik -RAA- akinukuliwa kusema kwamba, “Alikuwa akitembea na Mtume –SAW- na akapita kwa watoto na Mtume akawasalimia”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6247) na Muslim (2168).
Katika kuwsalamia watoto kuna: Kuifanya nafsi kuwa na unyenyekevu, na kuzoesha watoto waizowee nembo hii ya dini na kuifanya iwe hai katika nyoyo zao.
Na hii inaingia katika ujumla wa kusalimia. Na hayo ni baada ya kupiga mswaki, kwa sababu kupiga mswaki unapoingia nyumbani ni Suna. Hii ndio sehemu ya nne katika sehemu ambazo Suna ya kupiga mswaki inasisitizwa. Sehemu hiyo ni: Wakati wa kuingia nyumbani, kwa mujibu wa Hadithi ya Bi Aisha –RAA- katika mapokezi ya Muslim. Aisha amenukuliwa kusema kuwa: “Mtume –SAW- alikuwa anapoingia nyumbani kwake anaanza kwa kupiga mswaki”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (254). Mtume alikuwa akianza kuingia nyumbani kwake kwa kupiga mswaki kisha huingia na kuwasalamia waliomo humo. Baadhi ya Wanazuoni wamesema kuwa: Ni katika Suna kusalimia unapoingia kwenye nyumba yoyote, hata kama ndani ya nyumba hiyo hakuna mtu yeyote, kwa mujibu wa kauli ya Allah kwamba: {Na mtakapoingia majumbani salimianeni (kama kuna watu, na kama hakuna watu jisalimieni wenyewe); maamkizi kutoka kwa Allah, yenye Baraka, mazuri. Kama hivyo Allah anakubainishieni Aya ili mpate kutia akilini}. Sura Annuur, aya 61.
Ibnihajar- Allah amrehemu amesema kuwa: “Na inaingia katika ujumla wa kutangaza Salamu kwa mtu mwenye kuingia sehemu ambayo hakuna mtu yeyote, kwa mujibu wa kauli ya Aliyetukuka kwamba: {Na mtakapoingia majumbani toleaneni salamu (kama kuna watu, na kama hakuna watu jisalimieni wenyewe)}. Angalia: Fat-hulbaariy, Hadithi (6235), mlango wa kutoa Salamu.
Faida: Imepatikana kutoka katika maelezo yaliyopita kwamba kuna Suna za aina tatu wakati wa kuingia ndani nyumba:
Ya kwanza: Kutaja jina la Allah, na hasa usiku.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Jabir bin Abdallah -RAA- kwamba, alimusikia Mtume - SAW- akisema kuwa: “Mtu anapoingia nyumbani kwake, na akamtaja Allah wakati wa kuingia kwake, na wakati wa kula kwake, shetani husema (kuwaambia wenzake): Hakuna pa kulala leo wala chakula cha jioni. Na mtu anapoingia (nyumbani kwake) na hukumtaja Allah, shetani husema (kuwaambia wenzake): Mmepata pa kulala. Na kama hakumtaja Allah wakati wa kula kwake, shetani husema (kuwaambia wenzake): mmepata pa kulala, na chakula cha jioni”. Imepokewa na Muslim (2018).
Ya pili: Kupiga mswaki, kwa mujibu wa Hadithi ya Bibi Aisha –RAA- iliyotangulia kutajwa hapo nyuma.
Tatu: Kuwasalimia walioko nyumbani.
Na hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume-SAW- kama ilivyo katika Hadithi ya Mikidadi bin Al-as-wad- RAA-. Katika Hadithi hiyo, amesema Mikidadi kuwa: “……..Na tulikuwa tunakama na kila mtu anakunywa fungu lake, na tunampelekea Mtume-SAW- fungu lake. Akasema: Na (Mtume) anakuja usiku na anasalamia Salamu ambayo haimwamshi aliyelala, na aliye macho anaisikia”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2055).
Kufikisha Salamu ni Suna, kama vile mtu akuambie: “Nisalamie fulani”. Kwa hakika, ni katika Suna kwako kuifikisha Salamu hii kwa aliyesalimiwa.
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Aisha –RAA- kwamba, Mtume –SAW- alimwambia: “Hakika, Jibrili anakusalamia. (Aisha) Akasema: Na nikajibu: Na Amani na iwe ju yake na rehema za Allah”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (3217), na imepokewa na Muslim kwa nambari (2447).
Katika Hadithi hii kuna (maelekezo ya) kufikisha Salamu kwa aliyesalimiwa, kama Mtume -SAW- alivyofikisha Salamu za Jibrili -AS- kwa Bi Aisha-RAA-. Pia katika Hadithi hii iliyotangulia tunajifunza kwamba ni Suna kumtuma mtu apeleke Salamu.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema kwamba: “Anapoingia mmoja wenu katika kikao asalimie. Na anapotaka kuondoka asalamie, kwa sababu sio kwamba Salamu ya kwanza ina haki zaidi kuliko Salamu ya mwisho”. Ameipokea Ahmad kwa nambari (9664), Abudaudi kwa nambari (5208) na Tirmidhiy kwa nambari (2706). Shekh Albaniy amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Sahiihuljaami’u 1/132).
Na hivi ndivyo Swahaba, Allah awawie radhi, walivyokuwa wakifanya. Hoja ya hili ni: Hadithi ya Katada –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Nilimwambia Anas: Je, Swahaba wa Mtume walikuwa wanasalamiana kwa kupeana mikono? Akasema: Naam”. Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (6263).
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abudhari - RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, “Mtume-SAW- aliniambia: Usidharau jambo lolote katika mema, hata kama ni kukutana na ndugu yako kwa uso wa bashasha”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2626). Na kwa nukuu ya Tirmidhiy ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abudhari -RAA- imenukuliwa kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema kwamba: “Kutabasamu kwako katika uso wa ndugu yako ni sadaka kwako”. Imepokewa na Tirmidhiy kwa nambari (1956), na Shekh Albaniy amesema kuwa ni Hadithi sahihi. (Silisila Swahiha 572).
Ni sawa maneno mazuri hayo ni wakati wa kukutana, au kikaoni, au katika hali yeyote ile. Maneno mazuri ni Suna, kwa sababu ni sadaka.
Na hoja ya hili ni: Hadithi ya Abuhuraira - RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah -SAW- amesema kwamba: “Na maneno mazuri ni sadaka”.
Imepokewa na Bukhari, kwa nambari (2989), na Muslim kwa nambari (1009).
Na mara nyingi watu wamekuwa wakizungumza maneno mazuri. Lau kama wangenuia kupata thawabu wangelipwa kheri nyingi, na wangepata fungu kubwa la sadaka hizi.
Shekhe wetu Ibniuthaimini - Allah amrehemu - amesema kuwa: “Maneno mazuri ni kama kumwambia (mwenzako): Hujambo? Uhali gani? Vipi ndugu zako?”
Ihali gani familia yako? Na maneno mengine yanayofanana na hayo, kwa sababu haya ni katika maneno mazuri ambayo yanaingiza furaha kwa mwenzako. Kila neno zuri ni sadaka kwako mbele ya Allah, ni malipo na ni thawabu”. Angalia: Sharhu Riyaadhusswaalihiina ya Shekhe wetu (2/996), mlango wa: Kupendekezwa kwa maneno mazuri, na kuoneshana uso wa bashasha wakati wa kukutana.
Hadithi katika kuelezea fadhila za vikao vya kumtaja Allah, na kuhimiza hilo ni nyingi. Katika hizo ni Hadithi ya Abuhuraira - RAA- akinukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah-SAW-amesema kwamba: “Hakika, Allah ana Malaika wanaozunguka katika njia, wakitafuta watu wanaomtaja Allah. Wanapokuta watu wanaomtaja Allah huitana (na kuambiana): Njooni kwenye haja yenu (Mliyokuwa mkiitafuta). Mtume akasema: Watawafunika kwa mbawa zao mpaka katika uwingu wa dunia”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari: (6408) na Muslim kwa nambari (2689).
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira –RAA- akinukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah- SAW- amesema kwamba: “Atakayekaa katika kikao kikawa na kelele nyingi, na akasoma (dua ifuatayo) kabla ya kuondoka katika kikao chake hicho: “Sub-haanakallaahumma wabihamdika, Ash-hadu Allaa ilaaha illaa Anta, Astaghfiruka wa-atuubu ilayka”, “Umetakasika Ewe Mola wangu, na Himidi ni zako, Nakiri kuwa hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa wewe tu. Nakuomba maghfira (msamaha) na natubu kwako”. Atasamehewa yaliyotokea katika kikao chake hicho”. Imepokewa na Tirmidhi kwa nambari (3433), na Shekh Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi. Swahiihuljaamiu (2/1065).