NI KATIKA SUNA KUANZA MGUU WA KULIA KATIKA KUVAA VIATU.
Ni katika Suna Muislamu anapotaka kuvaa viatu vyake aanze na mguu wa kulia, na anapotaka kuvivua aanze na mguu wa kushoto.
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Abuhuraira –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema kwamba: “Mmoja wenu anapovaa viatu aanze kulia, na anapovua aanze kushoto. Mguu wa kulia uwe wa mwanzo kuvalishwa kiatu na uwe wa mwisho kuvuliwa”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5856).
Na katika matamshi mengine ya Muslim kuna nukuu kwamba: “Asitembee mmoja wenu akiwa kavaa kiatu kimoja. Yatakikana avae vyote au avivue vyote”.Imepokewa na Muslim kwa nambari (2097).
Katika Hadithi hizi mbili kuna Suna tatu:
1. Aanze mguu wa kulia wakati wa kuvaa viatu.
2. Aanze mguu wa kushoto wakati wa kuvua viatu.
3. Avae viatu vyote viwili au avue vyote, ili asitembee akiwa kava kiatu kimoja.
NI KATIKA SUNA KUVAA NGUO NYEUPE.
Linalokusudiwa ni kuvaa nguo ya rangi nyeupe, kwa sababu hiyo ni katika Suna, kwa mujibu wa Hadithi ya Ibniabbass –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –RAA- amesema kwamba: “Katika nguo zenu, vaeni nyeupe, kwa sababu hizo ndio nguo zenu bora zaidi, na muwakafini maiti wenu kwa nguo hizo”.Imepokewa na Ahmad kwa nambari (2219), Abudaudi kwa nambari (3878) na Tirmidhi kwa nambari (994). Shekh Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi. Swahiihulljaamiu (1/267).
Sheikh wetu Ibniuthamini -Allah amrehemu- amesema kuwa “Na (kauli) hiyo inajumuisha kuvaa nguo zote nyeupe kama vile: kanzu, vikoi, suruali. Zote hizo yatakikana ziwe nyeupe. Hilo ni bora zaidi. Lakini kama mtu atavaa nguo ya rangi nyingine hapana ubaya, kwa sharti kwamba nguo hiyo isiwe katika mavazi maalumu yanayovaliwa na wanawake”.Angalia: Sharhu Riyaadhusswaalihiin, ya Shekhe wetu (2/1087).
NI KATIKA SUNA KUTUMIA MANUKATO.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Anas –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema kwamba: “Katika dunia yenu nimefanywa kupenda wanawake na manukato, na burudani yangu imewekwa katika kuswali”.Imepokewa na Ahmad kwa nambari (12293), na Nasai kwa nambari (3940). Na amesema Shekhe Albani katika “Swahiih Annasaaiy” kuwa “Ni Hadithi Hassan (inayokubalika)”.
Ama matamshi: “Katika dunia yenunimefanywa kupenda vitu vitatu” ni dhaifu.
- Na Mtume - SAW- alikuwa anachukia kunuka harufu mbaya. Katika Hadithi ndefu iliyopokewa na Bukhari akimnukuu Bibi Aisha-RAA- kwamba, amesema kuwa: “Na ilikuwa ni jambo kubwa kwa Mtume wa Allah -SAW- kuwa ananuka harufu mbaya”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6972).
NI MAKURUHU KUKATAA MANUKATO.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Anas -RAA- aliyenukuliwa kusema kwamb, “Mtume –SAW- alikuwa hakatai manukato”.Imepokewa na Bukhari kwa nambari (2582).
NI KATIKA SUNA KUANZA NA UPANDE WA KULIA WAKATI WA KUCHANA NYWELE.
Ni katika Suna kuanza na upande wa kulia kisha upande wa kushoto katika kuchana nywele.
Na hoja ya hili ni:
Hadithi ya Aisha-RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, “Mtume wa Allah –SAW- alikuwa akipenda kuanza upande wa kulia katikaa kuvaa kwake viatu, kutembea kwake, kujitwaharisha kwake na katika kila mambo yake yote”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (168) na Muslim (268).
MAWASILIANO
SISI
TUNAFURAHISHWA KUWASILIANA KWAKO NA SISI NA MASWALI YAKO KWA WAKATI WOWOTE.