Imenukuliwa kwa Umar bin Abusalama – RAA – akisema kuwa: “Nilikuwa kijana mdogo chini ya ulezi wa Mtume wa Allah, na mkono wangu ulikuwa ukizungukazunguka hovyo katika sinia (ya chakula). Mtume wa Allah akaniambia: “Ewe kijana! Taja jina la Allaah na kula kwa mkono wako wa kulia, na ule kilicho mbele yako”. Basi huo ukawa ndio mtindo wangu wa kula baadaye. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5376) na Muslim (2022).
Na mtu akisahau kutaja jina la Allah: Ni Suna aseme pale anapokumbuka; “Bismillaahi Awwalahuu Wa-aakhirah”, ({nakula} Kwa jina Allah Mwanzo wake na mwisho wake).
Kwa mujibu wa Hadithi ya Aisha – RAA – kwamba, Mtume wa Allah–SAW-amesema kuwa: “Anapokula mmoja wenu ataje jina la Allah. Na akisahau kutaja jina la Allah mwanzo wake aseme: “Bismillaahi Awwalahuu Wa-aakhirah”. Imepokewa na Abudaud kwa nambari (3767) na Tirmidhi kwa nambari (1858). Na Shekh Albani amesema kuwa ni Hadithi sahihi, kama ilivyotangulia kuelezwa.
Pia Hadithi hii ni ushahidi kwamba, mwanadamu anatakiwa ale kwa mkono wake wa kulia ili asijifananishe na shetani. Muislamu anapokuwa hajataja jina la Allah, shetani hushirikiana naye katika chakula chake. Na anapokula au kunywa kwa mkono wake wa kushoto, anajifananisha na shetani kwa kufanya hivyo, kwa sababu shetani anakula na kunywa kwa mkono wake wa kushoto.
Na hoja ya hili ni:
Hadithi ya Abdallah bin Umar – RAA – kwamba, Mtume wa Allah–SAW-amesema kuwa: “Asile mmoja wenu kwa mkono wake wa kushoto, wala asinywe kwa mkono huo, kwa sababu Shetani anakula kwa mkono wake wa kushoto na anakunywa kwa mkono huo”. Na Imam Naafi alikuwa anazidisha: “Wala asipokee (kitu) kwa mkono huo (wa kushoto) na wala asitoe (kitu kumpa mtu) kwa mkono huo (wa kushoto)”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2020).
Na Shetani hutaka sana kuingia katika majumba ili alale humo na ashirikiane na watu wa majumba hayo chakula na kinywaji. Imepokewa kwa Jabir bin Abdallah- RAA- kwamba, alimsikia Mtume –SAW-akisema kuwa: “Mtu anapoingia nyumbani kwake au anapokula akamtaja Allah wakati wa kuingia kwake na wakati wa kula kwake, Shetani husema (kuwaambia mashetani wenzake kuwa): “Hmna mahali pa kukaa wala chakula”. Lakini mtu akiingia bila ya kumtaja Allah, Shetani husema (kuwaambia mashetani wenzake kuwa): “Mmepata mahali pa kukaa”. Na Muislamu asipomtaja Allah wakati wa kula, Shetani husema (kuwaambia mashetani wenzake kuwa): “Mmepata mahali pa kukaa na chakula”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2018).
Imenukuliwa kwa Umar bin Abusalama – RAA – akisema kuwa: “Nilikuwa kijana mdogo chini ya ulezi wa Mtume wa Allah, na mkono wangu ulikuwa ukizungukazunguka hovyo katika sinia (ya chakula). Mtume wa Allah akaniambia: “Ewe kijana! Taja jina la Allaah na kula kwa mkono wako wa kulia, na ule kilicho mbele yako”. Basi huo ukawa ndio mtindo wangu wa kula baadaye. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5376) na Muslim (2022).
Kwa mujibu wa Hadithi ya Jabir – RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, nilimsikia Mtume –SAW- akisema kwamba: “Hakika, Shetani anamuandama mmoja wenu katika kila jambo lake. Anamuandama hata kwenye chakula chake. Kwa hiyo, inapomuanguka mmoja wenu tonge ya chakula, aondoe sehemu iliyoingia taka na aile, na wala asimuachie shetani. Akimaliza (kula) arambe vidole vyake, kwa sababu mtu hajui baraka ipo katika chakula chake kipi”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2033).
Anayeiangalia Hadithi hii atakuta kwamba, Shetani ana shauku kubwa ya kutaka kushirikiana na mwanadamu katika mambo yake yote, ili aondoe baraka katika maisha yake, na amharibie mambo yake mengi. Miongoni mwa ushahidi unao onesha kuwa shetani anamuandama mja katika mambo yake yote ni kauli ya Mtume -SAW- isemayo kuwa: “Hakika, Shetani anamuandama mmoja wenu katika kila jambo lake”.
Na “Kuramba vidole” ni kaviramba kwa kutumia ulimi wake. Suna ni kuviramba, au kumrambsha mtu mwengine kama vile mkewe kwa mfano. Lakini Suna sio kupangusa chakula kinachobaki katika mkono wake kwa kitambaa, na mfano wake. Suna ni avirambe.
Na hoja ya hilo ni: Hadithi ya Jabir- RAA-iliyopita.
Na katika Sahiih Bukhararii na Sahiih Muslim kuna nukuu ambayo ni sehemu ya Hadithi ya Ibniabass –RAA- kwamba Mtume –SAW- amesema kuwa: “Anapokula mmoja wenu asifute mkono wake mpaka aurambe au aurambishe”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (5456) na Muslim kwa nambari (2033).
Makusudio ya kukomba sahani ni: Mlaji kusafisha eneo lake alilokulia chakula chake. Kwa mfano: Anayekula wali, ni katika Suna kutobakisha chochote katika eneo la sahani yake anayokulia. Anatakiwa apanguse kinachobaki katika sahani yake na akile, kwa sababu inaweza kuwa baraka ya chakula hicho iko katika hiki kilichobaki katika sahani yake.
Na hoja ya hilo ni Hadithi ya Anas -RAA- aliyenukuliwa kusema kwamba: “Na - Mtume –SAW- ametuamrisha kukomba (chakula kwenye) sahani”. Ameipokea Muslim kwa nambari (2034). Na katika upokezi wa Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira -RAA- kuna nukuu kwamba: “Na akombe mmoja wenu (chakula kwenye) sahani”. Ameipokea Muslim kwa nambari (2035).
Shekhe wetu Ibniuthaimin – Allah amrehemu – amesema kuwa: “(Suna hii ina maana kwamba: Ufuatilie chakula kilichobaki katika sahani kwa kutumia vidole vyako na uvirambe. Hii vilevile ni katika Suna ambazo, kwa masikitiko, watu wengi, hata wanazuoni, wamezipuuza, pia”. Angalia Sharhu Riyaadhusswaalihiin (1/892).
Na Suna ni kula kwa kutumia vidole vitatu. Hii ni katika vyakula vinavyochukulika kwa vidole vitatu, kama tende mfano. Ni Suna ale chakula cha aina hiyo kwa vidole vitatu.
Na hoja ya hili ni: Hadithi ya Kaabi bin Maalik -RAA-akinukuliwa kusema kuwa: “Mtume -SAW- alikuwa anakula kwa vidole vitatu, na anaramba mkono wake kabla ya kuupangusa”. Ameipokea Muslim kwa nambari: (2032).
Ni katika Suna kunywa kwenye chombo funda tatu, na apumue baada ya kila funda moja.
Na hoja ya hilo ni: Hadithi ya Anas –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume –SAW- alikuwa akipumua mara tatu katika kunywa kinywaji, na anasema: “Hakika, njia hiyo inakata kiu zaidi, na inapozesha zaidi, na inaburudisha zaidi”. Anas -RAA- amesema: “Mimi napumua mara tatu nikinywa kinywaji”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5631), na Muslim kwa nambari (2028).
Makusudio ya kupumua katika chombo ni: Kupumua wakati wa kunywa kwake katika chombo, kwa maana ya kwamba: anapumua nje ya chombo, kwa sababu kupumua ndani ya chombo ni makuruhu, kwa mujibu wa Hadithi ya Abukatada – RAA – iliopo katika Sahiih Bukhaariy na Sahiih Muslim kwamba, Mtume –SAW- amesema kuwa: “Anapokunywa mmoja wenu asipumulie ndani ya chombo”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5630) na Muslim kwa nambari (267).
Na hoja ya Suna hii ni:
Hadithi ya Anas bin Malik –RAA- aliyenukuliwa kusema kwamba, Mtume –SAW- amesema kuwa: “Hakika, Allah anamridhia mja alapo chakula kisha akamhimidi Allah kwa chakula hicho, au anywapo kinywaji kisha akamhimidi Allah kwa kinywaji hicho”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2743).
Kuhimidi kuna matamshi mbalimbali. Miongoni mwa hayo ni:
a. “Alhamdulillaahi Kathiiraa, Twayyiban, Mubaarakan Fiih, Ghayra Makfiiyyin Walaa Muwadda’in, Walaa Mustaghnaan ‘Anhu Rabbanaa”, (Sifa njema ni za Allah, sifa nyingi nzuri, zenye baraka ndani yake. Allah asiyetoshelezwa wala kususwa, wala kutohitajika Eee Mola wetu). Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5458).
b. “Alhamdulillaahilladhii Kafaanaa, Wa-arwaanaa, Ghayr Makfiyyin Wala Makfuur”, (Sifa Njema ni za Allah ambaye ametutosha, na ametuondoshea kiu, asiyetoshwa wala kukanwa). Imepokewa na Bukhari kwa nambari (5759).
(Asiyetoshwa) Inamaanisha asiyemhitaji yeyote. Yeye ndiye huwapa chakula waja wake na kuwatosheleza. (Kutengwa) Yaani: Haachwi. (Kafaanaa) Ametutosha. Na (Katuondoshea kiu) ametupa maji. (Kukanwa) hakuna wa kupinga fadhila na neema zake.
Ni katika Suna kujumuika kwa ajili ya chakula, na kutokaa mbalimbali.
Ushahidi wa hilo ni: Hadithi ya Jabir bin Abdallah -RAA- akinukuliwa kusema kuwa: “Nilimsikia Mtume wa Allah –SAW- akisema kuwa: “Chakula cha mtu mmoja kinawatosha watu wawili, na chakula cha watu wawili kinawatosha watu wanne, na chakula cha watu wanne kinawatosha watu wanane”. Imepokelewa na Muslim kwa nambari (2059).
Ni katika Suna mtu kukisifia chakula kikimpendeza. Na hakuna shaka kwamba mtu hakisifii chakula isipokuwa tu ni kwa sababu ya kilichomo ndani yake.
Na ushahidi wa hili ni: Hadithi ya Jabir bin Abdallah -RAA- kwamba, Mtume –SAW- alimuomba mke wake kitoweo, na wakasema: Hatuna isipokuwa siki tu. Akaomba apewe. Akawa anakula huku akisema: “Kitoweo bora ni siki. Kitoweo bora ni siki”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2052). Siki ni aina ya kitoweo chao (wakati huo) na ni tamu, sio chachu kama siki yetu hivi sasa.
Shekhe wetu Ibniuthaimini -Allah amrehemu- amesema kuwa: “Na hii pia ni katika mwongozo wa Mtume-SAW-kwamba, mtu akikipenda chakula akisifie. Kwa mfano: kama umevutiwa na mkate na ukataka kuusifia, unasema: Mkate mzuri ni mkate wa Fulani, au mfano wa maneno kama hayo. Hii nayo ni Suna ya Mtume –SAW-.” Angalia Sharhu Riyaadhusswaalihiin (2/1057).
Mwenye kuangalia hali yetu ya sasa atakuta kwamba, mara nyingi watu wanafanya tofauti na Suna ya Mtume. Sio kwamba wameacha Suna tu, lakini pia wanaipinga kwa kukitia ila chakula wakati mwingine, jambo ambalo ni kinyume na muongozo wa Mtume-SAW-. Katika Sahiih Bukhararii na Sahiih Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira –RAA- amenukuliwa kusema kuwa: “Mtume –SAW- katu hakukitia dosari chakula. Alipokipenda alikila na alipokuwa hakipendi alikiacha”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (3563) na Muslim kwa nambari (2064).
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Abdallah bin Busri - RAA-aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume –SAW- alikuja kwa baba yangu akiwa mgeni. Akasema (Abdallah bin Busri) kuwa: “Na tukamkaribisha (Mtume) chakula; tende na mseto (wa tende, maziwa yaliyokaushwa na samli), na akala. Kisha akaletewa tende, akawa anakula na kutupa kokwa zake kati ya vidole vyake, na anakunja kidole cha shahada na cha katikati. Kisha akaletewa kinywaji akanywa, na kisha akampa aliyekuwa upande wake wa kulia. Akasema (Abdallah bin Busri) kuwa: “Baba yangu akiwa ameshika hatamu ya mnyama wa Mtume na alimwambia (Mtume) kuwa: “Tuombee Mungu. Mtume akasema: “Ewe Allah, wabariki katika riziki uliyowapa, na wasamehe, na warehemu”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2042).
Mseto (huu): Ni aina ya chakula cha mchanganyiko wa tende, maziwa yaliyokaushwa na samli.
Kinachokusudiwa ni kuwa, ni katika Suna mtu akinywa ampe aliyepo upande wake wa kulia kabla ya aliyepo upande wa kushoto.
Na ushahidi juu ya hilo ni Hadithi ya Anas bin Malik-RAA- alinukuliwa kusema kuwa: “Alitujia Mtume –SAW- katika nyumba yetu. Akaomba kinywaji, na tukamkamulia mbuzi. Kisha nikachanganya maziwa (hayo ya mbuzi) na maji ya kisima changu hiki. Akasema Anas: Nikampa Mtume –SAW- na akanywa huku Abubakar akiwa kushotoni mwake, Umar akiwa mbele yake na Bedui mmoja akiwa upande wake wa kulia. Mtume wa Allah alipomaliza kunywa, Umar akamwambia Mtume: Huyu hapa Abubakar ewe Mtume wa Allah, akimwashiria. Mtume akampa Bedui, na kuwacha Abubakar na Umar, na kusema: Wa kuliani (kwanza). Wa kuliani (kwanza). Wa kuliani (kwanza)”. Akasema Anas –RAA-: “Hiyo ni Suna. Hiyo ni Suna. Hiyo ni Suna”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (2571) na Muslim kwa nambari (2029).
Ni Suna kwa mwenye kuwapa kinywaji watu awe wa mwisho wao kunywa.
Na hoja juu ya hilo: Ni Hadithi ndefu ya Abukatada –RAA-, na ndani ya Hadithi hiyo kuna nukuu kwamba: “Akawa Mtume –SAW- anajaza (kinywaji kwenye chombo) na mimi nawapa wanywe, mpaka ikawa hakubakia yeyote ila mimi tu na Mtume –SAW. Kisha Mtume –SAW- akajaza (chombo) na kuniambia “Kunywa”. Nikamwambia: “Hapana, sinywi mpaka unywe wewe (kwanza) ewe Mtume wa Allah. Akasema: “Hakika, mwenye kuwanywesha watu ndiyo wa mwisho wao kunywa”. Akasema Anas: Nikanywa na Mtume-SAW- naye akanywa”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (681).
Faida: Na ni katika Suna kwa mwenye kunywa maziwa asukutue kwa maji baada ya kunywa maziwa, ili aondoe lehemu iliyopo mdomoni mwake inayotokana na maziwa hayo. Na hoja ya hili ni Hadithi ya Ibniabass -RAA- akinukuliwa kusema kuwa: “Mtume – SAW - alikunywa maziwa kisha akaomba maji. Akasukutua na kusema: “Hakika, (maziwa) yana lehemu”. Imepokewa na Bukhari (211) na Muslim kwa nambari (358).
Ni Suna kufunika chombo ambacho kiko wazi wakati usiku unapoingia, na kufunika mitungi ya maji kama ina kifuniko, na kutaja jina la Allah wakati ukifanya hivyo.
Na hoja ya hilo ni Hadithi ya Jabir bin Abdallah -RAA-aliyenukuliwa kusema kuwa: “Nimemsikia Mtume wa Allah –SAW- akisema kuwa: Funikeni vyombo, na fungeni viriba. Hakika, katika mwaka kuna usiku mmoja ambao huteremka ndani yake ugonjwa. (Ugonjwa huo) Haukipitii chombo ambacho hakijafunikwa, au kiriba (mtungi) ambao hauna kifuniko, isipokuwa kwamba huingia humo”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2014). Na mapokezi ya Bukhari ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Jabir - RAA- pia kuna nukuu kwamba: “Na fungeni viriba vyenu, na tajeni jina la Allah, na funikeni vyombo vyenu na tajeni jina la Allah. (Funikeni) hata kama ni kwa kuwekea kitu (chochote) juu”. Imepokewa na Bukhari (5623).