Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhurara –Allah amridhie- akinukuliwa kusema kuwa, Mtume –SAW- amesema kwamba: “Lau watu wangelijua (fadhila) za kuwahi mapema msikitini wangeshindania (katika kuwahi msikitini)”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (615) na Muslim kwa nambari (437).
Kuwahi: Ni kwenda mapema kwa ajili ya Swala.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira –Allah amridhie- aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –SAW-amesema kwamba: “Mtu kuswali kwa Jamaa huzidi kuswali kwake nyumbani kwake, kuswali kwake sokoni kwake kwa daraja ishirini na ushei. Hiyo ni kwa sababu, mmoja wao anapotawadha vizuri kisha akenda msikitini, hakuna lililomuinua isipokuwa Swala tu, hakusudii isipokuwa Swala tu, basi (atakuwa) hapigi hatua isipokuwa atapandishwa daraja kwa hatua hiyo na ataondolewa dhambi kwa hatua hiyo mpaka aingie msikitini. Akishaingia msikitini, ataendelea kuwa katika Swala madamu Swala ndio iliyomzuia (kubaki humo msikitini). Na Malaika humuombea rehema mmoja wenu madamu yupo katika mahali pake aliposwali; wanaomba: Ewe Mola wetu, mrehemu. Ewe Mola wetu, msamehe. Ewe Mola wetu, mkubalie toba yake, (Hali inaendelea kuwa hivyo) madamu hajaudhi humo (msikitini) au kupatwa na Hadathi (kutengukwa na Udhu)”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (649).
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira – Allah amridhie – akimnukuu Mtume- SAW- kwamba amesema: “Mkisikia Ikama, tembeeni kwenda kuswali mkilazimika kuwa katika utulivu na upole, na msifanye haraka. Mtakacho kiwahi swalini, na kitachowapiteni kitimizeni”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (636) na Muslim kwa nambari (602).
Imamu Nawawiy, Allah amrehemu, amesema kuwa: “Upole maana yake ni kuwa mtaratibu katika kutenda na kujiepusha kuchezacheza. Utulivu ni katika muonekano, kama kuinamisha macho (kwa kutoangalia haramu) na kupunguza sauti (wakati wa kuzungumza) na kutogeukageuka”. Sharhu Sahih Muslim, Hadithi nambari (602), Mlango wa kupendekezwa kwa kwenda kuswali kwa utulivu na upole na kukatazwa kuiendea swala kwa kukimbia.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Anas – Allah amridhie – akinukuliwa kusema kuwa: “Ni katika Suna unapoingia msikitini uanze kwa mguu wako wa kulia, na unapotoka uanze kwa mguu wako wa kushoto”. Imepokewa na Hakim (1/388) na kusema kuwa ni sahihi kwa sharti ya Muslim.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhamiid, au Abu-usaid akinukuliwa kusema kuwa, Mtume – SAW – amesema kwamba: “Mmoja wenu anapoingia msikitini, aseme: Allaahumma Iftah Lii Ab-waaba Rahmatik (Ewe Mola wangu, nifungulie milango ya rehema zako), na anapotoka aseme: Allaahumma Innii As-Aluka Min Fadhwlik”, (Ewe Mola wangu, ninakuomba fadhila zako” Imepokewa na Muslim kwa nambari (713).
Na hii ni mtu anapokuja msikitini mapema. Ni suna kwake asikae mpaka aswali Rakaa mbili, kwa mujibu wa Hadithi ya Abukatada – Allah amuwie radhi – akinukuliwa kusema kuwa, Mtume – SAW – amesema kwamba “Mmoja wenu anapoingia Msikitini, asiketi mpaka aswali Rakaa mbili”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1163).
Na Suna ya Kabliya (sala ya Suna iliyopangiwa muda wa kabla ya sala ya faradhi) inatosheleza Tahiyyatul Masjid ikiwa Swala hiyo (ya Faradhi) ina Suna ya Kabliya, kama vile Swala ya Alfajiri na Adhuhuri, au Suna ya Dhuha ikiwa mtu ataingia msikitini wakati wa Dhuha, au Swala ya Witiri ikiwa mtu ataiswali msikitini, au swala ya faradhi. Hii ni kwa sababu, lengo la Tahiyyatul Masjid ni kuwa mtu asikae hadi aswali, kwa sababu katika kufanya hivyo kuna kuiimarisha misikiti kwa kuswali, ili mtu asije akawa anaingia misikitini na kutoka bila ya kuswali.
Ni Suna kwa wanaume kuwahi Safu ya kwanza, kwa Sababu ndio Safu bora zaidi. Na kwa wanawake Safu bora zaidi ni ya mwisho.
Kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira – Allah amridhie – aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume – SAW – amesema kwamba: “Safu bora zaidi ya wanaume ni Safu ya kwanza, na Safu mbaya zaidi ni Safu ya mwisho. Na Safu bora zaidi ya wanawake ni Safu ya mwisho, na Safu mbaya zaidi ya wanawake ni (Safu yao) ya kwanza”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (440). Maana ya Bora zaidi ni kwamba: Ina thawabu na fadhila nyingi sana. Na maana ya mbaya zaidi ni kwamba: Ina thawabu na fadhila chache sana.
Na Hadithi inalenga ni pale wanaume na wanawake watakaposwali pamoja; yaani kwa Jamaa, na hakuna kizuizi kati yao kama vile ukuta na mfano wake. Hapo, itakuwa safu bora ya wanawake ni safu ya mwisho, kwa sababu itakuwa ndio sitara zaidi kwao wasionekane na wanaume. Ama pale penye kizuizui kati ya safu za wanaume na wanawake, kama vile ukuta na mfano wake au kama ilivyo katika misikiti yetu mingi siku hizi ambapo wanawake wametengewa eneo maalumu lenye kujitegemea, katika hali hii safu bora zaidi ya wanawake ni safu ya kwanza, kwa sababu ya kukosekana kwa sababu ya kuwa karibu na wanaume. Hukumu huzunguka kufuata sababu yake kwa kuwepo na kwa kukosekana. Pia ni kwa sababu ya kuwepo kwa Hadithi kadhaa za jumla zinzoelezea ubora wa safu ya kwanza. Baadhi ya Hadithi hizo ni hizi zifuatazo:
Hadithi ya Abuhuraira – Allah amridhie – aliyenukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah –SAW- amesema kwamba: “Lau kama watu wangejua (faida, fadhila na mema) yaliyomo kwenye Adhana na safu ya kwanza, kisha wasipate (njia ya kupata nafasi ya kuwa katika safu ya kwanza) ila kwa kupiga kura, wangepiga kura. Na lau kama wangejua (faida, fadhila na mema) yaliyomo katika kwenda msikitini mapema, wangelishindania. Na lau kama wangelijua (faida, fadhila na mema) yaliyomo ndani ya Swala ya Alfajiri na Swala ya Isha wangeliziendea japo kwa kutambaa”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (615) na Muslim kwa nambari (437).
Iliyo bora kwa maamuma katika kusimama safu kwa ajili ya swala ni safu ya kwanza kama ilivyotangulia. Kisha awe na hamu ya kuwa karibu na imamu. Kuwa karibu zaidi (na imamu) kutoka upande wa kulia au wa kushoto ndio bora zaidi.
Na ushahidi wa hilo ni:
Hadithi ya Abdallah bin Masoud – Allah amridhie – akinukuliwa kusema kuwa, Mtume wa Allah-SAW-amesema kwamba: “Na wawe karibu yangu (wasimame karibu na mimi) miongoni mwenu wale wenye balehe na kupevuka akili”. Ameipokea Abudaud kwa nambari (674) na Tirmidhiy kwa nambari (228). Kauli ya Mtume kwamba: “wawe karibu yangu” ni hoja kwamba kuwa karibu na imamu ni jambo linalo takikana kwa upande wowote utakaokuwa.