Hilo ni kabla kuanza kutawadha, au kabla ya kusukutua. Hapa ndipo sehemu ya pili ambapo ni Suna kupiga mswaki, na sehemu ya kwanza imeshatangulia kutajwa. Ni Suna kwa anayetaka kutawadha apige mswaki, kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira –Allah amridhie- aliyenukuu kwamba, Mtume SAW amesema kuwa: “Lau nisingeona kuwa itakuwa mashaka (uzito) kwa Umma wangu ningewaamrisha kupiga mswaki wakati wa kila Udhu”. Hadithi hii imepokewa na Ahmad ikiwa na nambari (9928.) Pia imepokewa na Ibnikhuzaima na kutaja kuwa ni sahihi (1/73/140). Pia ameipokea Hakim (245/1) na Bukhari kwa Taaliq (kutotajwa kwa baadhi ya wapokezi) kwa lugha ya Jazmi (lugha ya kusisitiza usahihi wa Hadithi) katika mlango wa: “(Kutumia) Mswaki wa mti mbichi na mkavu kwa mwenye kufunga”.
Na kutokana na Hadith ya Aisha –Allah amridhie- aliyesema kuwa: “Tulikuwa tunamtayarishia (Mtume) mswaki wake na maji yake ya kujitwaharishia. Allah anampa ujumbe anaotaka kumpa usiku. Anapiga mswaki na anatawadha na anaswali”. Hadithi hii imepokewa na Muslim ikiwa na nambari (746).
Kutokana na Hadithi ya Uthman- Allah Amridhie- katika kuelezea namna ya Udhu wa Mtume SAW. Katika maelezo hayo kuna “(Mtume) Aliagiza aletewe chombo cha kutawadhia na akatawadha. Aliosha viganja vyake viwili mara tatu…”. Kisha (Uthman) akasema: “Nilimuona Mtume –SAW- akitawadha kama hivi nilivyotawadha”. Hadithi hii ameipokea Bukhari ikiwa na nambari (164) na Muslim kwa nambari (226).
Kutokana na Hadithi ya Aisha–Allah amridhie- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume- SAW-alikuwa anapenda sana kutumia upande wa kulia katika kuvaa viatu vyake, kuchana nywele zake na kujitwaharisha kwake na katika mambo yake yote”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1680) na Muslim kwa nambari (268).
Kwa Hadithi ya Uthman –Allah amridhie- katika kuelezea namna ya Udhu wa Mtume SAW kwamba “Alisukutua na akavuta maji puani, kisha akaosha uso wake mara tatu”. Hadithi hii imepokewa na Bukhari kwa nambari (199) na Muslim kwa nambari (226). Ikiwa mtu atachelewesha kusukutua na kuvuta maji puani (na kuyafanya hayo) baada ya kuosha uso itafaa.
Kutokana na Hadithi ya Lukait bin Swabra –Allah amridhie-aliyesimulia kwamba Mtume- SAW-alimwambia kuwa: ‘‘Tawadha vizuri na pitisha vidole kati ya vidole na zidisha katika kuvuta maji kwenye pua isipokuwa unapokuwa umefunga’’. Hadithi hii imepokewa na Ahmad kwa nambari (17846) na Abudaud kwa nambari (142). Amesema Ibnihajar kuwa: “Hii ni Hadithi sahihi”. Al-iswaba (9/15). Kuzidisha katika kusukutua kumepatikana kutoka katika kauli ya Mtume kwamba “Tawadha vizuri”.
Kutokana na Hadithi ya Abdallah bin Zaid – Allah amridhie- katika kuelezea namna Mtume alivyokuwa akitawadha na kusema kuwa: “……. (Mtume) Aliingiza mkono wake kisha akautoa. Alisukutua na kuvuta maji puani kwa kutumia kiganja kimoja. Alifanya hivyo mara tatu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (192) na Muslim kwa nambari (235).
Namna hiyo ni mtu kuanza katika kupaka maji kichwa chake kwa kuweka mikono yake mbele ya kichwa chake, kisha aipeleke mpaka kichogoni mwake. Kisha airejeshe pale mahali alipoanzia. Mwanamke pia anafanya Suna hii kwa njia hiyo hiyo. Nywele zilizozidi na kuwa nje ya shingo ya mwanamke hazipakwi maji.
USHAHIDI WA HILI NI:
Hadithi ya Abdallah bin Zaid - Allah amridhie – katika kuelezea namna Mtume SAW alivyokuwa akitawadha. Katika maelezo hayo kuna maneno haya: “(Mtume) Alianzia sehemu ya mbele ya kichwa chake kisha akaipeleka (mikono yake) mpaka kichogoni mwake. Kisha akairudisha mpaka pahali alipoanzia”. Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (185) na Muslim kwa nambari (235).
Mara ya kwanza ni wajibu. Ama mara ya pili na ya tatu ni Suna. Haitakiwi kuzidisha zaidi ya mara tatu.
USHAHIDI WA HILI NI:
Hadithi ya Ibniabbas –Allah amridhie yeye na baba yake - iliyothibitishwa na Bukhari -Allah amrehemu- “Kwamba Mtume –SAW-alitawadha mara moja mara moja’’. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (157). Na imethibiti kwa Bukhari pia ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abdallah bin Zaid –Allah amridhie-“Kwamba Mtume- SAW-alitawadha mara mbili mara mbili”. Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (158). Pia imethibiti katika Sahih Bukharin a Sahih Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Uthmaan –Allah amridhie- “Kwamba Mtume –SAW- alitawadha mara tatu tatu”. Ameipokea Bukhari kwa nambari (159). Kwa hivyo, ni bora kubadilisha saa nyingine. Mara atawadhe mara moja moja, wakati mwingine mara mbili mbili, wakati mwingine mara tatu tatu, na mara nyingine apishanishe idadi. Kwa mfano: aoshe uso mara tatu, mikono mara mbili mbili, na miguu mara moja moja, kama ilivyo katika Sahih Bukhari na Sahih Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abdallah bin Zaid-Allah amridhie- katika mapokezi mengine. Angalia: Zaadul Maad (1/192). Lakini, jambo la aghlabu zaidi ni mtu afanye kwa ukamilifu mara tatu tatu, kwa sababu huo ndio muongozo wa Mtume –SAW-.
Imenukuliwa kwa Umar –Allah amridhie- akisema kuwa, amesema Mtume wa Allah–SAW- kwamba: “Hakuna yeyote kati yenu anayetawadha akautimiza vilivyo Udhuu wake, kisha akasema: “Nashuhudia ya kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allah tu, na kwamba Muhammad ni Mja Wa Allah na Mtume Wake, (Ash-hadu Allaa ilaaha illa-llaah, Wa-ash-hadu Anna Muhammadan Abdullaahi Warasuuluhu) isipokuwa atafunguliwa milango minane ya pepo aingie kupitia mlango wowote autakao”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (234).
Au Dua iliyokuja katika Hadithi ya Abusaid–Allah amridhie- ikihusishwa na Mtume kwamba “Mwenye kutawadha kisha akamaliza Udhu wake na akasema: Sub-hanakallahumma Wabihamdik, Ash-hadu Allaa Ilaaha Illaa Anta, Astaghfiruka Wa-atuubu Ilayika, (Utukufu na sifa njema zote ni zako. Nashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila wewe tu. Naomba msamaha wako na natubu kwako), Allah hupiga muhuri na kuwekwa lakiri, kisha ikanyanyuliwa na kuwekwa chini ya Arshi na haitavunjwa lakiri hiyo mpaka siku ya Kiyama”. Imepokeleawa na Nasai katika Matendo ya Usiku na Mchana. (Ukurasa 147). Pia ameipokea Hakim (1/752) na Ibnihajar – Allah amrehemu-amesema kuwa orodha ya wapokezi wake ni sahihi. Angalia Nataa-ijul-afkaar, (1/246). Ameendelea kubainisha kuwa, kama sio sahihi kuihusisha kwa Mtume, basi imehusishwa kwa Swahaba. Hilo halina tatizo, kwa sababu jambo hilo linachukua hukumu ya kuhusishwa kwa Mtume, kwakuwa ni miongoni mwa mambo ambayo rai ya mtu haina nafasi katika mambo hayo.