Wakati wa Dhuha ni Suna Mja aswali Swala ya Dhuha.
Na ushahidi wake ni:
a. Hadithi ya Abuhuraira – RAA – amesema aliyenukuliwa kusema kuwa: “Ameniusia rafiki yangu (Swallallaahu ‘alayhi wasallam) mambo matatu: kufunga swaumu siku tatu katika kila mwezi, rakaa mbili za Dhuhaa na niswali Witiri kabla ya kulala”. Na pia Mtume – SAW -alimuusia mambo hayo Abudardai – RAA – (Muslim 722). na Abudhari – RAA – (Nasai – Assunan Alkubraa). Shekh Albani amesema kuwa Hadithi hii ni sahihi.
b. Hadithi ya Abudhari – RAA - akimnukuu Mtume –SAW- kwamba, amesema kuwa: “Panapopambazuka, inakuwepo sadaka katika kila kiungo cha mmoja wenu. Kila Tasbihi (Sub-haanallaah = Ametakasika Allah) ni Sadaka, na kila Tahmidi (Alhamdu Lillaah = Sifa njema ni za Allah) ni sadaka, na kila Tahalili (Laa ilaaha illallaah = Hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allah tu) ni sadaka, na kila Takbira (Allaahu Akbar= Allah ni Mkubwa zaidi) ni sadaka, na kuamrisha mema ni sadaka, na kukataza maovu ni sadaka. Na yote hayo yanatoshelezwa na rakaa mbili anazoswali mtu wakati wa Dhuha”.Imepokewa na Muslim kwa nambari (720).
Viungo: Ni sehemu ya mwili iliyojigawa.
Na umekuja ufafanuzi katika Sahihi Muslim ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Aisha – RAA – kwamba kila mwanadamu ameumbwa akiwa na viungo mia tatu na sitini, na kwamba mwenye kuleta idadi hii ya sadaka, atakuwa anatembea siku hiyo akiwa ameepushwa na moto wa Jahanamu.
Wakati wake
Wakati wa swala ya Dhuha unaanza pale jua linapoinuka kwa kadiri ya kiwango cha mkuki; kwa maana ya baada ya kutoka wakati uliokatazwa kuswali.
Na unakwisha: Muda mfupi kabla ya wakati wa Zawali (jua kupinduka kuacha usawa wa kati); kwa maana kabla ya kuingia wakati wa swala ya Adhuhuri kwa takribani dakika kumi.
Na hoja ya hili ni Hadithi ya Amri bin Absa – RAA -: “Swali swala ya asubuhi, kisha acha kuswali wakati jua linachomoza mpaka liinuke… Kisha swali, kwa sababu swala hiyo inashuhudiwa na inahudhuriwa, mpaka kivuli kitoshane na mkuki. Kisha acha kuswali wakati huo, kwa sababu wakati huo Jahanamu huwa inakokwa (inakolezwa)”. Ameipokea Muslim kwa nambari (832).
Wakati wake bora zaidi:
Ni katika wakati wake wa mwisho ambao ni pale kwato za ndama wa Ngamia zinapo ungua kwa jua kuwa kalili.
Na hoja yake ni Hadithi ya Zaid bin Arqam – RAA - pindi kwato za ndama wa ngamia zinapo ungua kwa sababu ya jua kuwa kali na kuchoma, kwamba Mtume – SAW – amesema (kuwa huo ndio muda wa): Swala ya wenye kutii”. Imepokewa na Muslimkwa nambari (748).
Ibnibaz - Allah amrehemu - amesema kuwa: “Maana ya kuchomo:
ni wakati joto la jua linapozidi. Na Ndama: Ni watoto wa ngamia. Swala hii ni katika zile swala ambazo kuziswali mwisho wa wakati ni bora zaidi. Angalia (Fataawaa Islaamiyya 1/515).
Idadi ya Rakaa zake:
Uchache wa swala ya Dhuha ni Rakaa mbili, kwa mujibu wa Hadithi ya Abuhuraira – RAA – iliopo katika Sahiih mbili (Sahiih Bukhaariy na Sahiih Mulim) akinukuliwa kusema kuwa: “Aliniusia rafiki yangu mambo matatu” na akataja katika hayo “na rakaa mbili za Dhuha”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1981), na Muslim kwa nambari (721).
Ama wingi wa swala ya Dhuha, lililo sahihi ni kwamba haina ukomo wa wingi wake, tofauti na wale walioiwekea ukomo wa rakaa nane. Kwa hiyo, mtu ana hiyari ya kuzidisha zaidi ya rakaa nane hadi kiasi ambacho Allah – SWT – atakachomuwezesha, kwa mujibu wa Hadithi ya Aisha – RAA – aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume – SAW - alikuwa anaswali Dhuha rakaa nne na anazidisha mpaka Allah atakavyo”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (719).
MAWASILIANO
SISI
TUNAFURAHISHWA KUWASILIANA KWAKO NA SISI NA MASWALI YAKO KWA WAKATI WOWOTE.