brightness_1
SUNA NI KUWA KAMA MWENYE KUPIGA CHAFYA HAJAMHIMIDI ALLAH, HAOMBEWI “YARAHAMUKA LLAAH”.
Kama mwenye kupiga chafya hajamhimidi Allah – sio katika Suna sisi kumuombea “Yarhamukallaah”, lakini Suna ni kutomuombea, kwa mujibu wa Hadithi ya Anas –RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Walipiga chafya watu wawili mbele ya Mtume –SAW-. Mmoja wao akahimidi Allah, na mwengine hakumhimidi Allah. Mtume alimuombea dua mmoja wao na mwengine hakumuombea. Akasema (yule ambaye hakuombewa dua) kwamba: Ewe Mtume wa Allah, umemuombea huyu na mimi hukuniombea. Mtume akasema: “Hakika, huyu amemhimidi Allah na wewe hukumhimidi Allah”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6225). Na hii ni katika kitendo cha Mtume - SAW-. Na katika kauli ya Mtume-SAW- imekuja Hadithi iliyopokewa na Muslim ikiwa ni nukuu kutoka kwa Abumusa aliyesema kuwa, Mtume –SAW- amesema kwamba: “Mmoja wenu atakapopiga chafya kisha akamhimidi Allah muombeeni dua (yaani mwambieni Yarhamukallaah). Na kama hakumhimidi Allah msimuombee dua (yaani msimwambie Yarhamukallaah)”. Ameipokea Muslim namba (2992).
Lakini inapokuwa mazingira ni ya kufundisha, kama vile baba kumlea mtoto wake, au mwalimu kuwafundisha wanafunzi wake, au mfano wa hivyo, hapo anaweza kumwambia: Sema “Alhamdulillah” ili amlee katika kuijua na kuitekeleza Suna hii, kwa sababu inawezekana akawa Suna hii haijui.
Pia yule aliye na ugonjwa wa mafua, haombewi dua ya “Yarhamukallaah” baada ya kupiga chafya mara ya tatu. Akipiga chafya mara ya tatu ataombewa dua ya “Yarhamukallaah”, na baada ya hapo hataombewa.
Na hoja ya hili ni: Ile Hadithi aliyoipokea Abudaudi katika kitabu chake cha Sunan ikiwa ni nukuu kwa Abuhuraira RAA- ikiwa Mawquuf (Iliyohusishwa na Swahaba tu) na Marfuu (iliyohusishwa na Mtume s.a.w.) kwamba: “Muombee ndugu yako aliyepiga chafya dua ya “Yarhamukallaah” mara tatu. Na ikizidi mara tatu huo ni ugonjwa wa mafua”. Imepokewa na Abudaudi kwa nambari (5034). Shekh Albani -Allah amrehemu- amesema kuwa Hadithi hii ni “Hasan (inakubalika) ikiwa Mauquuf (imehusishwa na Swahaba tu)” na ni “Hasan (inakubalika) ikiwa Marfuu (imehusishwa na Mtume)”. (Swahiih Abudaudi 4/308).
Na Hadithi hii inapewa nguvu na Hadithi iliyopokewa na Muslim katika kitabu chake cha Swahiih Muslim, ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Salama bin Ak-wai -RAA- kwamba, wakati kuna mtu alipiga chafya mbele ya Mtume, alimsikia Mtume –SAW- akimwambia: “Yarhamukallaah”. Kisha yule mtu akapiga chafya mara nyingine, Mtume –SAW akamwambia: “Mtu huyu ana mafua”. Ameipokea Muslim kwa nambari (2993).
Imebainika katika maelezo yaliyotangulia kuwa mwenye kupiga chafya haombewi dua ya “Yarhamukallaah” katika hali mbili:
1. Kama mpiga chafya hakusema “Alhamdulillaah”
2. Anapozidisha kupiga chafya mara tatu, kwa sababu atakuwa na Mafua.