brightness_1
Ni katika Suna mtu kuswali Swala ya usiku katika wakati wake ulio bora zaidi.
Ikiulizwa: Ni upi wakati bora zaidi wa swala ya usiku?
Jawabu ni hili: Inajulikana kuwa wakati wa Swala ya Witiri unaanza baada ya Swala ya Isha mpaka kuchomoza kwa Alfajiri. Kwa hivyo, mahali pa swala ya Witiri ni muda uliopo baina ya Swala ya Isha na ya Alfajiri.
USHAHIDI WA HILI NI:
Hadithi ya Aisha- Allah amridhie- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume wa Allah- SAW-alikuwa akiswali rakaa kumi na moja katika muda uliopo baina ya kumaliza Swala ya Isha mpaka Alfajiri, akitoa Salamu kati ya kila raka mbili. Na anafanya Witiri kwa (kuswali) rakaa moja.” Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (2031) na Muslim kwa nambari (7736).
-AMA WAKATI BORA ZAIDI WA SWALA YA USIKU NI: THELUTHI YA USIKU BAADA YA NUSU YAKE.
Kinachokusudiwa: Ni kwamba mwanadamu anagawanya usiku nusu nusu. Anasimama na kuswali katika theluthi ya nusu ya pili ya usiku na mwisho wa usiku analala. Yaani anasimama na kuswali katika sudusi (1/6) ya nne na ya tano kisha analala katika sudusi ya sita.
Ushahidi wa hili ni: Hadithi ya Abdallah bin Amri – Allah amridhie yeye na baba yake- aliyenukuliwa kusema kwamba, Mtume wa Allah– SAW-amesema kuwa: “Hakika Swaumu inayopendwa sana na Allah ni Swaumu ya (Mtume) Daudi –AS- na Swala inayopendwa sana na Allah ni Swala ya (Mtume) Daudi –AS-. Alikuwa akilala nusu ya usiku, na anainuka (na kuswali) theluthi yake, na analala sudusi yake. Na alikuwa akifunga siku moja na anafungua siku (ya pili). Imepokelewa na Bukhari namba (3420).
- KAMA MTU AKITAKA KUTEKELEZA SUNA HII, ANAUHESABU VIPI USIKU WAKE?
Anahesabu wakati kutoka kuzama kwa jua mpaka kuchomoza kwa alfajiri. Kisha anaugawanya usiku huo vipande sita. Vipande vitatu vya kwanza ndio nusu ya kwanza ya usiku. Anasimama baada yake. Hii ikiwa na maana kwamba anasimama katika sudusi ya nne na ya tano, kwa sababu hii inazingatiwa kuwa ni theluthi. Kisha analala katika sudusi ya mwisho ambayo ndio sudusi ya sita. Kwa sababu hii Aisha –Allah- amesema kuwa: “Haukumfikia Mtume- SAW- wakati wa Sahar (Usiku wa Manani) akiwa kwangu isipokuwa alikuwa amelala.” Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1133) na Muslim kwa nambari (742).
Na kwa njia hii, Mwislamu anakuwa katika wakati bora sana wa kuswali usiku, kama ilivyokuja katika Hadithi iliyotangulia kutajwa ya Abdallah bin Amri- Allah amridhie yeye na baba yake.
UFUPI WA MANENO NI KWAMBA: UBORA KATIKA WAKATI WA KISIMAMO CHA USIKU UKO KATIKA DARAJA TATU:
Daraja ya kwanza: Ni mtu alale nusu ya kwanza ya usiku, kisha ainuke theluthi yake, kisha alale sudusi yake, kama ilivyotangulia kuelezwa.
Ushahidi wa hili ni: Hadithi ya Abdalla bin Amri bin Al-aas –Allah amridhie yeye na baba yake- ambayo imetangulia kutajwa hivi punde.
Daraja ya pili: Ni mtu aamke katika theluthi ya mwisho ya usiku.
Ushahidi wa haya ni:
Hadithi ya Abuhuraira –Allah amridhie- kwamba Mtume –SAW- amesema kuwa: “Mola wetu aliyetukuka na kutakasika anashuka kila usiku hadi mbingu ya chini kabisa, pale inapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Anasema: Ni nani anayeniita nimwitikie? Na ni nani anayeniomba nimpe? Na ni nani anayeniomba msamaha nimsamehe”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1145) na Muslim kwa nambari (758). Na pia kuna Hadithi ya Jabir- Allah amridhie- na itakuja.
Mtu akiogopa kuwa atashindwa kuamka mwishoni mwa usiku, basi aswali mwanzo wake au katika wakati wowote ambao utakuwa mwepesi kwake. Na hii ndio daraja ya tatu.
Daraja ya Tatu: Mtu anaswali wakati wa mwanzo wa usiku, au katika sehemu ya usiku ambayo ni nyepesi kwake.
Ushahidi wa hilo ni:
Hadithi ya Jabir –Allah amridhie- aliyesema kuwa, amesema Mtume wa Allah - SAW- kwamba: “Atakayechelea kutoamka mwisho wa usiku, basi aswali Witiri mwanzo wake. Na atakayetaraji kuamka mwisho wake basi aswali Witiri mwisho wa usiku, kwa sababu Swala ya mwisho wa usiku ni yenye kushuhudiwa, na hiyo ni bora zaidi”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (755).
Na vilevile unachukuliwa juu ya hili Wasia wa Mtume -SAW- kwa 1)Abudhari (imepokewa na Nasai katika Sunan Kub’ra (2712) na Albani ameisahihisha (Aswahiihatu (2166). na Wasika wa Mtume kwa 2)Abudrdaa (ameipokea Ahmad kwa kwa nambari (27481), na Abudaudi kwa kwa nambari (1433) na Albani ameisahihisha (Swahiih Abudaud nambari 5/177) na Wasia wa Mtume kwa 3)Abuhuraira –Allah amridhie- ameipokea Muslim kwa nambari (737). Kila mmoja (katika Swahaba hao) amenukuliwa akisema kuwa: “Ameniusia Kipenzi changu (Mtume) mambo matatu”, na akataja katika hayo: “Na (Aliniusia) niswali Witiri kabla sijalala”.