languageIcon
search
search
brightness_1 Ni katika Suna mtu kuswali Swala ya usiku katika wakati wake ulio bora zaidi.

Ikiulizwa: Ni upi wakati bora zaidi wa swala ya usiku?

Jawabu ni hili: Inajulikana kuwa wakati wa Swala ya Witiri unaanza baada ya Swala ya Isha mpaka kuchomoza kwa Alfajiri. Kwa hivyo, mahali pa swala ya Witiri ni muda uliopo baina ya Swala ya Isha na ya Alfajiri.

USHAHIDI WA HILI NI:

Hadithi ya Aisha- Allah amridhie- aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume wa Allah- SAW-alikuwa akiswali rakaa kumi na moja katika muda uliopo baina ya kumaliza Swala ya Isha mpaka Alfajiri, akitoa Salamu kati ya kila raka mbili. Na anafanya Witiri kwa (kuswali) rakaa moja.”  Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (2031) na Muslim kwa nambari (7736).

-AMA WAKATI BORA ZAIDI WA SWALA YA USIKU NI: THELUTHI YA USIKU BAADA YA NUSU YAKE.

Kinachokusudiwa: Ni kwamba mwanadamu anagawanya usiku nusu nusu. Anasimama na kuswali katika theluthi ya nusu ya pili ya usiku na mwisho wa usiku analala. Yaani anasimama na kuswali katika sudusi (1/6) ya nne na ya tano kisha analala katika sudusi ya sita.   

Ushahidi wa hili ni: Hadithi ya Abdallah bin Amri – Allah amridhie yeye na baba yake- aliyenukuliwa kusema kwamba, Mtume wa Allah– SAW-amesema kuwa: “Hakika Swaumu inayopendwa sana na Allah ni Swaumu ya (Mtume) Daudi –AS- na Swala inayopendwa sana na Allah ni Swala ya (Mtume) Daudi –AS-. Alikuwa akilala nusu ya usiku, na anainuka (na kuswali) theluthi yake, na analala sudusi yake. Na alikuwa akifunga siku moja na anafungua siku (ya pili). Imepokelewa na Bukhari namba (3420).

- KAMA MTU AKITAKA KUTEKELEZA SUNA HII, ANAUHESABU VIPI USIKU WAKE?

Anahesabu wakati kutoka kuzama kwa jua mpaka kuchomoza kwa alfajiri. Kisha anaugawanya usiku huo vipande sita. Vipande vitatu vya kwanza ndio nusu ya kwanza ya usiku. Anasimama baada yake. Hii ikiwa na maana kwamba anasimama katika sudusi ya nne na ya tano, kwa sababu hii inazingatiwa kuwa ni theluthi. Kisha analala katika sudusi ya mwisho ambayo ndio sudusi ya sita.  Kwa sababu hii Aisha –Allah- amesema kuwa: “Haukumfikia Mtume- SAW- wakati wa Sahar (Usiku wa Manani) akiwa kwangu isipokuwa alikuwa amelala.”  Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1133) na Muslim kwa nambari (742).

Na kwa njia hii, Mwislamu anakuwa katika wakati bora sana wa kuswali usiku, kama ilivyokuja katika Hadithi iliyotangulia kutajwa ya Abdallah bin Amri- Allah amridhie yeye na baba yake.

UFUPI WA MANENO NI KWAMBA: UBORA KATIKA WAKATI WA KISIMAMO CHA USIKU UKO KATIKA DARAJA TATU:

Daraja ya kwanza: Ni mtu alale nusu ya kwanza ya usiku, kisha ainuke theluthi yake, kisha alale sudusi yake, kama ilivyotangulia kuelezwa.

Ushahidi wa hili ni: Hadithi ya Abdalla bin Amri bin Al-aas –Allah amridhie yeye na baba yake- ambayo imetangulia kutajwa hivi punde.

Daraja ya pili: Ni mtu aamke katika theluthi ya mwisho ya usiku.

Ushahidi wa haya ni:

Hadithi ya Abuhuraira –Allah amridhie- kwamba Mtume –SAW- amesema kuwa: “Mola wetu aliyetukuka na kutakasika anashuka kila usiku hadi mbingu ya chini kabisa, pale inapobaki theluthi ya mwisho ya usiku. Anasema: Ni nani anayeniita nimwitikie? Na ni nani anayeniomba nimpe? Na ni nani anayeniomba msamaha nimsamehe”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (1145) na Muslim kwa nambari (758). Na pia kuna Hadithi ya Jabir- Allah amridhie- na itakuja.

Mtu akiogopa kuwa atashindwa kuamka mwishoni mwa usiku, basi aswali mwanzo wake au katika wakati wowote ambao utakuwa mwepesi kwake. Na hii ndio daraja ya tatu.

Daraja ya Tatu: Mtu anaswali wakati wa mwanzo wa usiku, au katika sehemu ya usiku ambayo ni nyepesi kwake.

Ushahidi wa hilo ni:

Hadithi ya Jabir –Allah amridhie- aliyesema kuwa, amesema Mtume wa Allah - SAW- kwamba: “Atakayechelea kutoamka mwisho wa usiku, basi aswali Witiri mwanzo wake. Na atakayetaraji kuamka mwisho wake basi aswali Witiri mwisho wa usiku, kwa sababu Swala ya mwisho wa usiku ni yenye kushuhudiwa, na hiyo ni bora zaidi”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (755).

Na vilevile unachukuliwa juu ya hili Wasia wa Mtume -SAW- kwa 1)Abudhari (imepokewa na Nasai katika Sunan Kub’ra (2712) na Albani ameisahihisha (Aswahiihatu (2166). na Wasika wa Mtume kwa 2)Abudrdaa (ameipokea Ahmad kwa kwa nambari (27481), na Abudaudi kwa kwa nambari (1433) na Albani ameisahihisha (Swahiih Abudaud nambari 5/177) na Wasia wa Mtume kwa 3)Abuhuraira –Allah amridhie- ameipokea Muslim kwa nambari (737). Kila mmoja (katika Swahaba hao) amenukuliwa akisema kuwa: “Ameniusia Kipenzi changu (Mtume) mambo matatu”, na akataja katika hayo: “Na (Aliniusia) niswali Witiri kabla sijalala”.

brightness_1 Ni katika Suna mtu kusoma dua za kuanzia swala zilizothibiti katika Swala ya usiku.

Ni katika Suna mtu kusoma dua za kuanzia swala zilizothibiti katika Swala ya usiku. Miongoni mwa dua hizo ni hizi:

a. Hadithi ya Aisha –Allah amridhie-iliyokuja katika Swahihi Muslim akinukuliwa kusema kuwa: “Mtume- SAW- anaposwali usiku anafungua swala yake kwa kusoma: Allaahumma Rabba Jibraa-iil wa Miikaa-iil wa Israafiil. Faatwiras-samaawaati wal-ardhwi. Aalimal ghaybi wash-shahaadah. Anta Tahkmu bayna ibaadika fiimaa kaanuu fiihi yakhtalifuun. Ihdinii limakhtulifa fiihi minalhaqqi Bi-idhnika. Innaka Tahdii Mantashaa-u ilaa Swiraatwim-mustaqiim. (Ee Allah, Mola wa Jibrili   na Mikaili na Israfili, Muumba wa mbingu na ardhi, Mjuzi wa ghaibu (yasiyo onekana kwa macho) na dhahiri, Wewe Utahukumu baina ya waja wako katika ambayo walikuwa wakihitilafiana. Niongoze mimi kwenye haki katika yale ambayo (watu) wamehitilafiana kwa idhini yako.  Hakika, wewe unamuongoza umtakae kwenye njia ilio nyooka). Imepokewa na Muslim kwa nambari (770).

b. Hadithi ya Ibniabbas –Allah amridhie yeye na baba yake- iliyokuja katika Swahih Bukhari na Swahih Muslim) aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume- SAW- anapofanya Tahajudi usiku alikuwa anasema: “Allaahumma Lakalhamdu. Anta Nuurussamaawaati Wal-ardhi. Walakalamdu. Anta Qayyimussamaawaati Wal-ardhi. Walakalhamdu. Anta Rabbussamaawaati Wal-ardhi Waman Fiihinna. Antalhaqqu. Waqaulukalhaqqu. Waliqaa-ukalhaqqu. Waljannatu Haqqun. Wannaaru Haqqun. Wannabiyyuuna Haqqun. Wassaa’tu Haqqun. Allahumma Laka Aslamtu. Wabika Aamantu. Wa-alaika Tawakkaltu. Wa-ilaika Anabtu. Wabika Khaaswamtu. Wa-ilaika Haakamtu. Faghfir Lii Maaqaddamtu, Wamaa Akh-khartu, Wamaa Asrartu, Wamaa A’alantu. Anta Ilaahii.  Laa Ilaaha Illaa Anta”.  (Ewe Allah, ni zako wewe tu sifa njema. Wewe ndiye nuru ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na ni zako wewe tu sifa njema. Wewe ndiye Mwenye kuzisimamia mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na ni zako wewe tu sifa njema. Wewe ni Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake.  Na sifa njema ni zako wewe tu. Wewe ni kweli, na ahadi yako ni ya kweli, na neno lako ni la kweli, na kukutana nawe ni kweli, na Pepo ni kweli, na Moto ni kweli, na Mitume ni kweli na Kiyama ni kweli. Ewe Mola wangu, kwako tu nimejisalimisha, na wewe tu nimekuamini, na wewe tu nimekutegemea, na kwa sababu yako tu nimegombana, na sheria zako tu nimezifuata. Nisamehe nilyokwishayafanya na nitakayoyafanya na niliyoyafanya kwa siri na niliyoyafanya dhahiri. Wewe ndiye Mola wangu. Hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa wewe tu). Imepokewa na Bukhari kwa nambari (7499) na Muslim kwa nambari (768).

brightness_1 Alete Suna zilizopokewa katika kisomo chake.

Alete Suna zilizopokewa katika kisomo chake. Miongoni mwa Suna hizo ni hizi:

a. Asome taratibu. Makusudio yake ni kuwa, mtu asiwe mwenye kwenda mbio katika kisomo.

b. Akate kisomo chake aya baada ya aya.  Maksudio ni kwamba: Mtu asiwe mwenye kuunganisha aya mbili au tatu bila kusimama. Bali awe anasimama katika kila aya.

c. Akipita katika aya ya Tasbihi analeta Tasbihi (Sub-haanallah), na akipita katika aya ya maombi anaomba, na akipita katika aya ya kuomba kinga anaomba kinga (kwa Allah) amlinde.

Na ushahidi wa hayo yaliyotangulia ni:

Hadithi ya Hudhaifa- Allah amridhie- aliyenukuliwa kuesema kuwa: “Niliswali na Mtume –SAW-usiku mmoja. Alianza kusoma Sura Albaqara nikasema: Atarukuu akifika aya ya mia moja. Kisha akapita, nikasema: Ataswali kwayo katika rakaa moja, na akapita. Nikasema: Atarukuu kwayo. Kisha akaanza (kusoma) Sura Annisaa na akaisoma (yote). Kisha akaanza (kusoma) Sura Aal-imrani na akaisoma (yote) kwa utulivu. Akipita kwenye aya ambayo ndani yake ina kusabihi anasabihi, na akipita kwenye aya ya kuomba anaomba, na akipita kwenye aya ya kuomba kinga anaomba kinga (kwa Allah). Kisha akarukuu akawa anasema: “Sub-haana Rabbiyal-adhwiim”. Kurukuu kwake kulikuwa kama kusimama kwake. Kasha akasema: “Samia-llaahu Liman Hamidah”, (Allah amemsikia mwenye kumhimidi). Kisha akasimama sana, kukaribia vile alivyorukuu. Kisha akasujudu na kusema: “Subhaana Rabiiyal A’alaa(Ametakasika Mola wangu Aliye Juu). Kusujudu kwake kulikuwa kunakaribia kusimama kwake. Ameipokea Muslim kwa nambari (772).  

Pia hayo ni kwa mujibu wa Hadithi ya Ummusalama –Allah amridhie- aliyoipokea Imam Ahmad –Allah amrehemu- katika kitabu chake cha Musnad, kwamba “(Ummu Salama) Aliulizwa kuhusu kisomo cha Mtume –SAW- akasema: Alikuwa akikata kisomo chake aya aya. (Bismillahirrahmaanirrahiim* Alhamdulillaahi Rabbil-aalamiin* Arrahmaanirrahiim* Maaliki Yaumiddiin)”. Imepokewa na Imam Ahmad (26583). Amesema Daarqutni kuwa (118): “Isnadi (Orodha ya wapokeaji wa Hadithi hii) ni sahihi na wote ni waaminifu”. Pia Imam Nawawi amesema kuwa ni sahihi (Almajmuu 3/333).

brightness_1 NI KATIKA SUNA WAKATI MWINGINE MTU KULETA KUNUTI KATIKA WITIRI YAKE.

Na makusudio yake hapa ni: Dua. Kunuti hiyo inafanyika katika Rakaa ya tatu ambayo mtu anasoma ndani yake Suratul Ikhlaasw.

Na Kunuti katika Witiri ni katika Suna wakati mwingine kuifanya, kwa sababu ya kuthibiti kwake kunukuliwa kwa baadhi ya Swahaba– Allah awawie radhi. Pia ni Suna kuiacha wakati mwingine. Sheikhul Islaam Ibnitaymia -Allah amrehemu- amelichagua hili (la kuacha kukunuti). Jambo bora zaidi ni kwamba kuacha Kunuti iwe ni kwingi zaidi kuliko kuileta.

  • : JE, YAFAA KUINUA MIKONO KATIKA KUNUTI YA WITIRI?

Iliyo sahihi ni kwamba: Mtu ananyanyua mikono. Wanazuoni wengi - Allah awarehemu - wamesema hivyo, kwa sababu ya kuthibiti kunukuliwa hilo kwa Ibniumar –Allah amridhie yeye na baba yake-, kama ilivyo kwa Baihaki ambaye amesema kuwa ni sahihi.

Baihaki –Allah amrehemu- amesema kuwa “Hakika, idadi (kadhaa) ya Swahaba –Allah awawie radhi- waliinua mikono yao katika Kunuti”. Angalia: Assunan Alkubraa (2/211).

  • : Kwa kitu gani mtu anaanza Kunuti yake katika Witiri?

Kauli yenye nguvu – na Allah ndiye mjuzi zaidi - ni kwamba, anaanza kwa kumhimidi Allah na kumsifu, kisha anamswalia Mtume-SAW-.  Kisha anaomba dua, kwa sababu hii iko karibu zaidi kujibiwa.

Ushahidi wa hilo ni:

Hadithi ya Fudhala bin Ubaid – Allah amridhie – aliyenukuliwa kusema kuwa: “Mtume–SAW-alimsikia mtu mmoja akiomba dua katika swala yake hali ya kuwa hakumswalia Mtume-SAW-, Mtume-SAW-akasema: “Huyu ameharakisha. Kisha alimuita na kumwambia yeye na wengine kwamba: “Mmoja wenu anaposwali, aanze kwa kumhimidi Allah na kumsifu, kisha aniswalie na aombe akitakacho baada ya hapo”.  Imepokewa na Tirmidhi kwa namba (3477), na akasema: Hii ni Hadithi nzuri na sahihi. 

Na Ibniqayyim – Allah amrehemu – amesema kuwa: “Kinachopendekezwa katika dua ni mwenye kuomba aanze kwa kumhimidi Allah na kumsifu kwa shida yake, kisha aombe shida yake, kama ilivyo katika Hadithi ya Fudhala bin Ubaid. Angalia: Alwaabilus-swayyib (Ukurasa wa110).

  • : JE, MTU ANAFUTA USO WAKE KWA MIKONO YAKE BAADA YA DUA YA KUNUTI?

Lililo sahihi ni kwamba: Sio Suna kupangusa uso baada ya kumaliza dua, kwa sababu ya kukosekana kwa hoja sahihi juu ya jambo hilo.

Imamu Malik - Allah amrehemu - aliulizwa kuhusu mtu anayefuta au kupangusa uso wake kwa mikono yake wakati wa kuomba dua, alilikanusha hilo na kusema “Silijui (hilo)”. Angalia kitabu cha Witri cha Maruuzi (Ukurasa wa 237).

Sheikh wa Uilamu Ibnitaimia – Allah amrehemu – amesema kuwa: “Ama mtu kupangusa uso wake kwa mikono yake hakuna isipokuwa Hadithi moja au mbili ambazo hoja haziwezi kusimama kama hoja”. Angalia: Fatawa (22/519).