languageIcon
search
search
brightness_1 ALLAH AMEHIMIZA KUTAJWA KATIKA MAENEO MENGI. MIONGONI MWA MAENEO HAYO NI:

1/ Allah amewahimiza waja wake wamtaje sana. Amesema :} Enyi mlioamini, mtajeni sana Allah, na mtakaseni asubuhi na jioni. (Sura Al-ahzaab 41: 42).

2/ Allah Mtukufu amewaahidi wenye kumtaja, wake kwa waume, kwamba atawapa msamaha, thawabu na malipo makubwa. Amesema: {Na wanaume wanaomtaja Allaah kwa wingi na wanawake, Allah amewaandalia maghufira na malipo makubwa}. (Sura Al-ahzaab: 35).

3/Na Allah -SWT- ametuhadharisha sifa za wanafiki. Wao wanamtaja Allah -SWT-, lakini hebu tafakari kiwango chao cha kumtajaji. Amesema Allah -SWT- kuwa: {Hakika, wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allah, na hali yeye (Allah) ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionesha kwa watu na wala hawamtaji Allah isipokuwa kidogo tu}. (Annisaa: 142).

4/ Allah –SWT- ametuhadharisha juu ya kushugulishwa na mali na watoto tukapuuza kumdhukuru. Amesema Allah aliyetukuka kuwa: {Enyi mlioamini, zisikupuuzisheni mali zenu na watoto wenu mkaacha kumdhukuru Allah. Na yeyote atakayefanya hivyo basi hao tu ndio waliohasirika}  (Sura Almunaafiquun: 9).

5/ Hebu tafakari pamoja nami huu ujira mkubwa na utukufu wa hali ya juu kabisa! Amesema Allah -SWT- kuwa: {Basi nitajeni na Mimi nitakukumbukeni}. Na Allah amesema katika Hadithi Kudusi kwamba: “Mimi niko vile mja wangu anavyonidhania. Niko pamoja naye anaponitaja. Anaponitaja katika nafsi yake, name namtaja katika nafsi yangu. Anaponitaja katika hadhara, nami namtaja katika hadhara bora zaidi kuliko hadhara yao”.  Imepokewa na Bukhari kwa nambari (7405), na Muslim kwa nambari (2675) ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira.

brightness_1 Na aina za nyiradi za kumtaja Allah zilizopokewa katika Suna ya Mtume -SAW- ni nyingi. Miongoni mwa niyiradi hizo ni hizi zifuatazo: (1)

1. Imenukuliwa kwa Abuhuraira -RAA- kwamba, Mtume –SAW- amesema kuwa: “Mwenye kusema: “Laa ilaaha illallaah Wahdahuu Laashariika Lah, Lahulmulku, Walahulhamdu, Wahuwa Alaa Kulli Shay-in Qadiir. (Hakuna Muabudiwa kwa haki ila Allah peke yake, hana mshirika. Ni wake yeye tu ufalme na ni zake yeye tu Sifa njema, na yeye ni Muweza wa kila kitu) mara mia moja kwa siku, atakuwa na ujira wa sawa na kuacha huru watumwa kumi, na ataandikiwa mema mia moja, na atafutiwa madhambi mia moja, na atakuwa na kinga dhidi ya shetani kwa siku yake hiyo, mpaka afikiwe na jioni. Na hatakuja mtu yeyote Siku ya Kiyama na kilicho bora zaidi ya alichokuja nacho yeye, isipokuwa tu yule aliyesema mfano wa hayo aliyosema au akazidisha juu ya hayo.  Na mwenye kusema: Sub-haanallaah wabihamdihii (Ametakasika Allah na sifa zote njema ni zake) mara mia moja kwa siku, atasamehewa dhambi zake hata kama ziko (nyingi) kama povu la bahari”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (3293), na Muslim kwa nambari (2691).

2. Na imenukuliwa kwa Abuayoub -RAA- akisema kuwa, amesema, Mtume –SAW- kwamba: “Mwenye kusema: “Laa ilaaha ilallaah Wahdahuu Laashariika Lah, Lahulmulku, Walahulamdu, Wahuwa Alaa Kulli Shay-in Qadiiru (Hakuna Muabudiwa kwa haki ila Allah peke yake, hana mshirika. Ni wake yeye tu ufalme na ni zake yeye tu Sifa njema, na yeye ni Muweza wa kila kitu) mara kumi, atakuwa kama aliyeacha huru watumwa wanne katika watoto wa Ismaili”.  Imepokewa na Bukhaari kwa nambari (6404) na Muslim kwa nambari (2693).

brightness_1 Na aina za nyiradi za kumtaja Allah zilizopokewa katika Suna ya Mtume -SAW- ni nyingi. Miongoni mwa niyiradi hizo ni hizi zifuatazo: (2)

3. Na imenukuliwa kwa Saad bin Abiwakas –RAA- akisema kuwa: “Tulikuwa mbele ya Mtume-SAW- akasema: Hivi anashindwa mmoja wenu kuchuma kila siku mema elfu moja? Muulizaji katika wale waliokuwa wameketi katika kikao kile akamuuliza Mtume: Atapataje mmoja wetu hayo mema elfu moja? Mtume akasema: Asabihi Tasibihi mia moja (yaani aseme Sub-haanallaah mara mia moja). Akifanya hivyo, ataandikiwa mema elfu moja au atafutiwa madhambi elfu moja”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2698).

4. Imenukuliwa kwa Abuhuraira -RAA- kwamba, Mtume-SAW- amesema kuwa: “Mwenye kusema Sub-haanallaah wabihamdihii (Ametakasika Allah na sifa zote njema ni zake) mara mia moja kwa siku, ataghufuriwa makosa yake japokuwa ni (mengi) mfano wa povu la bahari.” Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6405), na Muslim kwa nambari (2692). Na katika mapokezi ya Muslim kuna nukuu kwamba: “Mwenye kusema Sub-haanallaah wabihamdihii (Ametakasika Allah na sifa zote njema ni zake) mara mia moja asubuhi na jioni, hatakuja mtu yeyote Siku ya Kiyama na kilicho bora zaidi ya alichokuja nacho yeye isipokuwa yule aliyesema mfano wa hayo aliyosema au akazidisha juu ya hayo”.  Imepokewa na Muslim kwa nambari (2692).

Na Hadithi katika kuelezea aina za nyiradi na fadhila zake ziko nyingi. Hizo zilizotangulia kutajwa ni katika nyiradi sahihi na mashuhuri zaidi, lakini zipo nyingine nyingi zilizonukuliwa.  Imenukuliwa kwa Abumousa Al-ashari -RAA- akisema kuwa, amesema Mtume-SAW-: “Je nikufahamishe hazina miongoni mwa hazina za peponi?, Nikasema: Naam.  Mtume akasema: “Sema: Laa Hawla Walaa Quwwata illaa Billaah”, (Hakuna uwezo (wa kufanya mema) wala mbinu (za kuacha maovu) ila kwa msaada wa Allah tu).  Imepokewa na Bukhari kwa nambari (4202), na Muslim kwa nambari (2704).

Na imenukuliwa kwa Abuhuraira –RAA- akisema kuwa, amesema Mtume -SAW- kwamba: “Kwa yakini kabisa, kusema kwangu: Sub-haanallaah, Walhamdulillaah, walaa ilaaha illallaah, wallaahu Akbar- Utakasifu ni wa Allah na himdi anazistahiki Allah, na hakuna Muabudiwa wa haki ila Allah tu, na Allah ni Mkubwa; kusema hayo ni bora kwangu kuliko kila kilichoangaziwa na jua”. Imepokewa na Muslim kwa nambari (2695).

brightness_1 Na aina za nyiradi za kumtaja Allah zilizopokewa katika Suna ya Mtume -SAW- ni nyingi. Miongoni mwa niyiradi hizo ni hizi zifuatazo: (3)

Kumuomba msamaha Allah ni aina ya uradi pia. Imepokewa kwa Aghari Almuzani –RAA- akisema kuwa, amesema Mtume –SAW- kwamba: “Hakika mimi (kama mwanadamu) moyo wangu hushughulishwa (na mambo mbalimbali ya kidunia). Na mimi, kwa hakika, namuomba msamaha Allah kwa siku mara mia moja”.  Imepokewa na Muslim kwa nambari (2702).

Huu ni ushahidi wa Mtume-SAW- alivyokuwa yeye mwenyewe akiomba msamaha. Pia amehimiza, kwa maneno yake, kuomba msamaha kama ilivyo katika Swahiih Muslim ikinukuliwa kwa Aghari -RAA- pia kwamba, amesema Mtume –SAW- kuwa: “Enyi watu, tubuni kwa Allah. Hakika, mimi natubu kwa Allah kwa siku mara mia moja”.  Imepokewa na Muslim kwa nambari (2702).

Na katika upokezi wa Bukhaari ikiwa ni sehemu ya Hadithi ya Abuhuraira -RAA- imenukuliwa kuwa amesema: “Nimemsikia Mtume wa Allah (Rehema na amani ya Allah iwe juu yake) akisema:  Nina apa kwa Allah kwamba mimi namuomba msamaha Allah na natubu kwake zaidi ya mara sabini katika siku moja”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6307). Inampasa mja kutopuuza kumuomba Allah msamaha.

Na namalizia Suna ya kumtaja Allah - na pia Suna zote za kila siku- kwa kutaja uradi mkubwa uliopokewa katika Swahiih Bukhaarii na Swahiih Muslim. Ni Hadithi ya Abuhuraira- RAA- aliyenukuliwa kusema kuwa, amesema Mtume –SAW- kwamba: “Maneno mawili ni mepesi juu ya ulimi, ni mazito katika mizani, yanapendwa na (Allah) Mwingi wa rehema. Ni:  Sub-haanallaah Wabihamdihii, Sub-haanallahil-adhwiim”: “Ametakasika Allah, na sifa njema ni zake. Ametakasika Allah   aliye Mtukufu”. Imepokewa na Bukhari kwa nambari (6406), na Muslim kwa nambari (2694).

SIFA ZOTE NJEMA NI ZA ALLAH AMBAYE KWA NEEMA ZAKE MAMBO MEMA YANATIMIA.